Muungano wa Matatu nchini umeongoza maandamano ya amani mjini Mombasa, yakilenga kuwakumbuka waathiriwa wa ajali za barabarani na kuongeza msisitizo juu ya utekelezaji wa sheria za usalama barabarani. Hafla hiyo imewashirikisha madereva, makondakta, abiria, maafisa wa usalama, na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi wa umma, huku ikiwa na ujumbe wa uwajibikaji na kutii kanuni za barabarani.
Akihutubia wanahabari, Afisa Mkuu wa Idara ya Kupambana na majanga kaunti ya Mombasa, Ibrahim Abdallah Basafar, amesema idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani bado ni ya juu, akibainisha kuwa watu 4,500 wamepoteza maisha tangu mwanzo wa mwaka huu.
“Watumizi wa barabara wanapaswa kuwa makini ili kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha yao. Kuna haja ya kuzingatia sheria za barabarani ili kupunguza ajali.”amesema Basafar.

Kwa upande wake, naibu mwenyekiti wa chama cha matatu nchini, Ali Salim, amesisitiza umuhimu wa kudumisha nidhamu na utiifu wa sheria miongoni mwa waendeshaji vyombo vya usafiri pamoja na abiria.
“Nawahimiza waendeshaji na abiria wa matatu kudumisha nidhamu na kuzingatia sheria zilizoko.” Salim amesema.
Aidha, meneja wa NTSA ukanda wa pwani ametoa wito wa wajibu wa pamoja kwa watumiaji wa barabara na kusema kuwa jukumu la usalama ni la kila mmoja na wala sio maafisa wa trafiki pekee.
“Kila mmoja ana wajibu wa kutekeleza ili kujilinda na kuwalinda wengine barabarani.” Meneja wa NTSA amesema, huku akiongeza kuwa shirika hilo litaimarisha ufuatiliaji wa sheria hasa msimu wa sikukuu. Katika nukuu ya pili alisema, “NTSA itahakikisha sheria za barabarani zimezingatiwa kikamilifu huku tukizidisha juhudi wakati huu wa shamra shamra za msimu wa likizo.” ameongeza meneja wa NTSA.

Maandamano hayo yameelezwa kuwa sehemu ya kampeni za kuahamasisha umma kuhusu umuhimu wa uhai, usalama na uangalifu barabarani, huku wadau wakiahidi kuendeleza mikakati ya kupunguza vifo na majeruhi yanayotokana na ajali za barabarani.
NA HARRISON KAZUNGU.