Baraza la Kitaifa la Kiislamu humu nchini (SUPKEM) limejitokeza na kukanusha madai yanayosambazwa kuhusu uchaguzi wa uongozi wa Baraza hilo, likiyataja madai hayo kuwa ya kupotosha, hayana msingi na yanayoenezwa na watu wasiokuwa wanachama halali wa SUPKEM.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari jijini Mombasa, Makamu Mwenyekiti wa Kitaifa Seyyid Muhdhar Sharrif Khitamy, akiwa ameandamana na Mratibu wa Mkoa wa SUPKEM Sheikh Khamis Juma Nwaguzo, amesema madai ya walalamishi yanalenga kudhoofisha uongozi uliopo na kuingiza mgawanyiko ndani ya Baraza.
“Madai yanayoenezwa ni ya kupotosha na hayana msingi. Wanaoyasambaza hawana uhusiano wa kisheria wala uanachama na SUPKEM,” amesema Sheikh Khamis Juma Mwaguzo.

Kwa upande wake, Seyyid Muhdhar Sharrif Khitamy amesema kuwa uchaguzi wa mwisho wa SUPKEM uliandaliwa mwaka 2017, ambapo viongozi waliochaguliwa wakiongozwa na Al-Hajj Hassan Ole Naado wameleta mafanikio makubwa, licha ya changamoto wanazokumbana nazo.
“Uongozi wa sasa umefanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Jaribio la kuibua taharuki ni hatua ya kujaribu kuzuia safari ya maendeleo chini ya Ole Naado,” amesema Khitamy.
Ameongeza kuwa Baraza hilo lipo ofisini na linafanya kazi kisheria, na kwamba juhudi zinazoonekana sasa ni njama za kuzua taharuki, vurugu na kupotosha umma kuhusu uhalali wa uongozi uliopo.
“Tunawahimiza Waislamu nchini kudumisha amani, mshikamano na utii wa sheria,” amesisitiza Khitamy .
Baraza hilo limewataka walalamishi kufuata taratibu za kisheria, ikiwezekana kujiandaa kwa uchaguzi wa majimbo badala ya kueneza uvumi, chuki na taharuki ndani ya jamii.
NA HARRISON KAZUNGU.