SERIKALI YAONGOZA JUHUDI ZA KUWAFARIJI NA KUUNGA MKONO WAATHIRIWA WA MAPOROMOKO YA ARDHI ELGEYO MARAKWET.
By Dayo Radio
Published on 08/11/2025 19:47
News

Serikali inaendelea kuongoza juhudi za uokoaji, urejeshaji wa hali, na misaada ya kibinadamu kufuatia janga la maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo idadi ya waliofariki imesalia 37, watu 9 wamelazwa hospitalini wakipokea matibabu na ushauri wa kisaikolojia, huku 11 wakiwa bado hawajapatikana.

Mama wa Taifa, mama Rachel Ruto, ametembelea eneo lililoathirika akiwa ameandamana na waziri wa usalama wa ndani na utawala wa kitaifa, Kipchumba Murkomen, waziri wa uchukuzi, Davis Chirchir, Waziri wa Utumishi wa umma, maendeleo ya rasilimali watu na mipango maalum, Geoffrey Ruku, Gavana wa Kaunti ya Nandi, Stephen Sang, na Gavana wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Wesley Rotich.

Hata hivyo Mama Rachel ametoa ujumbe wa faraja kutoka kwa Rais William Ruto, akisisitiza dhamira ya serikali kuwasaidia waathiriwa kurejesha maisha yao. 

 

Aidhs Viongozi hao wamehusika katika kugawa chakula na misaada kwa familia zilizoathirika, ikiwemo michango kutoka muungano wa Kanda ya North Rift (NOREB), makanisa, mashirika ya kijamii, na wafanyabiashara wa Nandi.

 

Kwa upande wake mama wa taifa amehimiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na ushirikiano wa jamii katika kuhifadhi maeneo ya milima, na ameahidi kushiriki binafsi katika juhudi za upandaji miti na urejeshaji wa mazingira.

 

“Ni jukumu letu kama wananchi kulinda mazingira yetu. Nitaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha miti inapandwa na milima yetu inalindwa. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kujenga ustahimilivu wa tabianchi na kurejesha mandhari ya nchi,” amesema Mama Rachel Ruto.

 

Kwa upande wake, waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen, amefichua kuwa serikali imeanzisha mpango wa mwezi mmoja wa hatua za pamoja, ikiwemo uhakiki wa orodha za wahanga halisi, uimarishaji wa usalama, na marekebisho ya barabara ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali imeweka mpango wa mwezi mmoja kuhakikisha kila mwathiriwa anafikiwa na kusaidiwa ipasavyo. Tutahakikisha barabara zote muhimu zinakarabatiwa ili ziweze kustahimili majanga ya hali ya hewa,” amesema waziri Kipchumba Murkomen.

 

Waziri wa uchukuzi, Davis Chirchir, amesisitiza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo, huku akifichua kuwa serikali imelipa asilimia 80 ya madeni ya wakandarasi ili kuharakisha miradi ya barabara nchini.

“Amani ni sharti la maendeleo. Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 104, sawa na asilimia 80 ya madeni yote ya wakandarasi, ili kuhakikisha miradi ya barabara inaendelea kwa kasi nchini,” amesema Waziri Davis Chirchir.

 

Waziri wa utumishi wa umma, Geoffrey Ruku, amesema serikali italipa bili zote za hospitali, kufanikisha mazishi ya heshima kwa waliopoteza maisha na kusaidia familia kujijenga upya.

 

“Serikali imedhamiria kuwalipa bili zote za hospitali, kuhakikisha mazishi ya heshima, na kusaidia familia zilizopoteza makazi kurejea katika hali ya kawaida,” amesema Waziri Geoffrey Ruku.

 

Aidha, Gavana wa Elgeyo Marakwet, Wesley Rotich, amethibitisha kuwa majeruhi wanapokea matibabu bora katika Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH), ambapo zaidi ya watu 400 wamepatiwa huduma za afya kupitia kambi maalum ya matibabu kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO).

 

“Tunashukuru serikali kuu na washirika wa afya kama WHO kwa kuleta huduma za haraka kupitia kambi maalum. Zaidi ya watu 400 wamepata matibabu muhimu, jambo lililookoa maisha mengi,” amesema Gavana Wesley Rotich.

 

Vile vile Serikali imetangaza kuwa mazishi ya pamoja kwa waathiriwa yatafanyika tarehe 21 Novemba 2025, ili kutoa heshima na maziko ya heshima kwa wote waliopoteza maisha.

huku ikisisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha uokoaji, ujenzi upya wa maisha, na utekelezaji wa hatua za kudumu za kukabiliana na majanga kama haya.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!