Shirika la ajira la BrighterMonday Kenya, kwa ushirikiano na Mastercard Foundation, limezindua ripoti mpya inayofahamika kama Skills Gap and Gender Analysis Report 2025, ikibainisha mwelekeo wa soko la ajira nchini, changamoto za ujuzi, na fursa zinazowangoja vijana katika enzi ya kazi za kidijitali.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya wako chini ya umri wa miaka 35, hali inayoifanya nguvu kazi ya taifa kutegemea vijana, huku asilimia 62.1 ya waajiri wakilalamikia kutokuwepo kwa uwiano kati ya ujuzi wa wahitimu na mahitaji ya soko la ajira, jambo linalodhihirisha pengo kubwa la ujuzi linalohitaji mikakati mipya ya kielimu na kitaalamu.
Mkurugenzi Mkuu wa BrighterMonday Kenya, Bi. Sarah Ndegwa, amesema ripoti hiyo ni wito wa kuchukua hatua madhubuti katika kubadilisha mfumo wa mafunzo nchini,

“Tunapaswa kuhakikisha vijana, hasa wanawake, watu wenye ulemavu, na wale wa maeneo ya vijijini, wanapata mafunzo yanayowaandaa kwa ajira za kesho. Tumejitolea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi, na wadau wengine kuboresha mitaala, kuimarisha ushirikiano na taasisi za TVET, na kukuza mafunzo kwa vitendo yatakayowapa vijana ujuzi wa vitendo na ajira zenye heshima,” amesema Bi. Ndegwa.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa ujuzi wa kidijitali na teknolojia ndio unaotafutwa zaidi na waajiri nchini, ambapo asilimia 75.9 wameutaja kuwa muhimu katika sekta zote, huku ujuzi wa mawasiliano, kazi kwa pamoja, na utatuzi wa changamoto ukitajwa kuwa nyenzo kuu kwa mafanikio kazini.
Hata hivyo, ripoti imeonya kuhusu pengo la kidijitali linalozidi kuongezeka, kwani takriban asilimia 90 ya waajiri hutumia majukwaa ya kidijitali kama LinkedIn kutafuta wafanyakazi, lakini ni vijana asilimia 25 pekee kutoka maeneo yasiyo ya mijini wanaopata huduma bora ya intaneti, hali ambayo imewaweka nyuma wanawake, watu wenye ulemavu, na wakimbizi katika kupata nafasi za ajira.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, suluhisho ni pamoja na kuunda mitaala inayoendana na mahitaji ya soko la sasa, kuongeza ujuzi wa kidijitali na upatikanaji wa intaneti nchini kote, kukuza ajira za ngazi ya kaunti ili kupunguza tofauti za kieneo, na kuimarisha ushirikiano kati ya waajiri, taasisi za TVET, na mashirika ya vijana.
Kupitia mpango wake wa Generation Kazi, shirika la BrighterMonday Kenya limeendelea kuwajengea vijana wenye umri wa miaka 18–35 uwezo wa kitaaluma na nafasi za kujiajiri, likilenga zaidi wanawake (70%), vijana wa vijijini (70%), na watu wenye ulemavu (10%).
Ripoti hii ya pili chini ya mpango wa HR Smart Lab 2 imesisitiza dhamira ya shirika la BrighterMonday Kenya kuendelea kuwa nguzo ya tafiti za soko la ajira, na mshirika mkuu wa maendeleo ya nguvu kazi jumuishi, yenye ujuzi, na tayari kwa ajira za kesho.
NA HARRISON KAZUNGU.