TAASISI YA MASOROVEYA YAONYA DHIDI YA UZEMBE WA KUKABILI MAJANGA YA ARDHI.
By Dayo Radio
Published on 05/11/2025 16:27
News

Taasisi ya Masoroveya humu nchini (Institution of Surveyors of Kenya – ISK) imetoa wito kwa Serikali na wadau wa mazingira kuchukua hatua za dharura na za kudumu kukabiliana na athari za maporomoko ya ardhi, hasa katika maeneo hatarishi kama Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari rais wa taasisi hiyo Eric Nyadimo, taasisi hiyo imetoa salamu za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki waliofiwa, kujeruhiwa au kupoteza makazi kutokana na mkasa huo wa hivi karibuni.

Nyadimo amesema kuwa janga la Elgeyo Marakwet ni kumbusho chungu la hatari kubwa inayowakabili jamii zinazoishi katika maeneo yenye uwezekano mkubwa wa maporomoko ya ardhi, na ni ishara tosha kwamba taifa linahitaji kuchukua hatua za kitaifa za kuimarisha mipango ya kukabiliana na majanga na usimamizi endelevu wa ardhi.

Ameeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa maisha yamepotea licha ya onyo la mapema lililotolewa na Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, kutokana na ukosefu wa mipango thabiti ya uokoaji, miundombinu duni na kutokuwepo kwa kambi za muda kwa wakazi wa maeneo hatarishi.

 

Nyadimo ameongeza kuwa ukataji miti ovyo, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na upangaji duni wa makazi vimechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa matukio ya maporomoko ya ardhi nchini. Amesema kuwa juhudi za Serikali za kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032 ni za kupongezwa, lakini akasisitiza kwamba mpango huo unapaswa kuambatana na utekelezaji madhubuti wa sheria za matumizi bora ya ardhi, uhifadhi wa misitu na udhibiti wa makazi ili kufanikisha malengo hayo.

Taasisi hiyo pia imetoa mapendekezo kadhaa kwa Serikali, ikiwemo kushirikiana na taasisi za kitaalamu kama ISK katika kutekeleza uchoraji wa ramani za kijiografia ili kubaini maeneo hatarishi, kuimarisha maandalizi ya kukabili majanga kwa kuunganisha mifumo ya onyo la mapema na hatua za haraka za jamii, pamoja na kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kuhusu uhifadhi wa mazingira na makazi salama.

Aidha, ISK imeitaka Serikali kuimarisha mikakati ya kudhibiti ya ujenzi na makazi katika maeneo hatarishi, kurejesha misitu na vyanzo vya maji, na kuhakikisha sheria za matumizi ya ardhi zinatekelezwa ipasavyo.

Vilevile amesisitiza kuwa ni lazima taifa lichukulie mkasa huu kama funzo na mwito wa kuchukua hatua za haraka, akisema,

“Tuitumie janga hili kama funzo la taifa kutanguliza uhifadhi wa mazingira, upangaji wa matumizi ya ardhi kwa uangalifu, na hatua za kuzuia majanga si kwa kuwakumbuka waliopoteza maisha pekee, bali kwa kulinda maisha ya vizazi vijavyo.”

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!