MWENYEKITI WA MRADI WA LAPSET, ALI MENZA MBOGO, ASHIRIKI SHEREHE YA MAHAFALI YA FIRST BORN ACADEMY LIKONI.
By Dayo Radio
Published on 05/11/2025 16:02
News

Mwenyekiti wa mradi wa Lamu Port South Sudan Ethiopia Transport Corridor (LAPSSET), Ali Menza Mbogo, ameungana na wanafunzi, wazazi wa shule ya First Born Academy pamoja na wakazi wa Wadi ya Timwani,eneobunge la Likoniya katika hafla ya kuvutia ya mahafali iliyokuwa na furaha tele na kuashiria hatua muhimu katika safari ya elimu ya watoto wa eneo hilo.

Katika hotuba yake, Mbogo amesema kuwa ameendelea kuwa mtiifu na mwenye ari kubwa katika kuhimiza maendeleo ya elimu, akieleza kwamba sekta hiyo ni injini kuu ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Amesema kuwa kupitia elimu, watoto wanapata maarifa, maadili, na uwezo wa kujenga maisha bora kwao na kwa jamii wanamoishi.

Mbogo, ambaye pia ni kiongozi mwenye dira ya maendeleo ya kijamii, ameweka wazi kuwa kuboresha mazingira ya elimu ni sehemu ya ajenda yake ya muda mrefu ya kuinua hadhi ya Mombasa kupitia uwekezaji katika rasilimali watu. Ameeleza kuwa, kuwekeza katika elimu ni sawa na kuwekeza katika mustakabali wa taifa, kwani watoto wa leo ndio viongozi wa kesho.

Katika kuonyesha dhamira yake ya kusaidia sekta ya elimu, Mbogo amewazawadia wanafunzi wote wa shule hiyo vitabu vya kujifunzia ili kusaidia kupunguza mzigo wa kifedha kwa wazazi na kuhakikisha kuwa watoto wanaendelea kusoma bila changamoto za vifaa vya masomo. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wake wa kuunga mkono taasisi za elimu hasa zile zinazohudumia watoto kutoka jamii zenye uhitaji mkubwa.

“Ninaamini kuwa kila mtoto anastahili fursa sawa ya kupata elimu bora bila kujali hali yake ya kifedha. Tunapowekeza katika elimu, tunaleta mabadiliko chanya katika jamii zetu na kujenga kizazi chenye maadili, nidhamu na uwezo wa kubadili taifa,” amesema Mbogo huku akishangiliwa na wazazi na walimu waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo.

Mbogo pia amewahimiza wazazi, walimu na jamii nzima kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuwalea na kuwasaidia watoto kufikia ndoto zao, akisisitiza kuwa mafanikio ya taifa lolote hutegemea misingi ya elimu bora. Amepongeza uongozi wa shule ya First Born Academy kwa kujitolea kuboresha kiwango cha elimu na kuandaa wanafunzi walio na maadili mema, akisema kuwa juhudi hizo zinastahili kuungwa mkono na wadau wote.

Amehitimisha kwa kuahidi kuendelea kuwekeza katika miradi ya kijamii, hasa ile inayolenga kuinua elimu na kuwapa vijana fursa za maendeleo, akisema kuwa ndoto yake ni kuona kila mtoto wa Mombasa akipata elimu bora itakayomwezesha kuwa sehemu ya maendeleo endelevu ya taifa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!