SERIKALI YAHAIDI MSAADA KAMILI KWA FAMILIA ZILIZOATHIRIKA NA MAPOROMOKO YA UDONGO MARAKWET MASHARIKI.
By Dayo Radio
Published on 03/11/2025 13:47
News

Serikali imeahidi kutoa msaada kamili kwa familia zilizoathiriwa na maporomoko ya udongo katika eneo la Marakwet Mashariki, kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo watu 22 wamethibitishwa kufariki dunia huku takriban watu 29 wakiripotiwa kutoweka.

Msemaji wa Serikali, Dkt. Isaac Mwaura, amesema juhudi za uokoaji zinaendelea kwa ushirikiano wa mashirika mbalimbali ya kitaifa na kaunti, ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Huduma ya Polisi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Akizungumza na wanahabari, Dkt. Mwaura amesema serikali imejitolea kuhakikisha kuwa kila manusura wa janga hilo anapata msaada wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu.

Amesema serikali imeweka nguvu za pamoja kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma akisisitiza kuwa msaada unawafikia walioathirika kwa haraka.

“Serikali imejitolea kuhakikisha kuwa kila manusura wa janga hili anapata msaada wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu. Tumeweka nguvu za pamoja kuhakikisha hakuna anayesalia nyuma,” ameeleza Dkt. Mwaura.

Ameongeza kuwa tayari manusura 21, wakiwemo watu wazima 14 na watoto 7, wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Eldoret kwa matibabu.

Vile vile, Dkt. Mwaura amesisitiza kuwa serikali imeweka mikakati mahsusi kuhakikisha mitihani ya kitaifa inayoendelea katika shule zilizoathirika na janga hilo inafanyika bila changamoto yoyote.

“Tunataka kuwahakikishia wazazi na wanafunzi kuwa serikali imechukua hatua zote muhimu ili mitihani iendelee kama ilivyopangwa licha ya changamoto zilizojitokeza,” amenukuliwa akisema.

Aidha, amewataka wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu na kushirikiana na maafisa wa usalama pamoja na wahudumu wa misaada wakati juhudi za uokoaji na utoaji wa misaada zikiendelea.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!