VIJANA ZAIDI YA ELFU TATU KISAUNI WANUFAIKA NA MRADI WA MASKANI YETU FOR PEACE.
By Dayo Radio
Published on 31/10/2025 18:20
News

Zaidi ya vijana elfu tatu katika eneo bunge la Kisauni sasa wamepata kituo kipya cha kujumuika, kujadili masuala yanayowahusu na kujiendeleza kimaisha kupitia mradi wa Maskani Yetu for Peace uliozinduliwa rasmi na shirika la kijamii la AMAKENI CBO.

Mradi huo unalenga kuwa kimbilio salama kwa vijana kwa kuwapa nafasi ya kujitenga na fikra potofu za kihalifu na badala yake kushiriki katika shughuli za kujenga jamii, kukuza talanta na kuimarisha uchumi wao kupitia miradi bunifu.

Akizungumza wakati wa hafla ya kujadiliana kuhusu mambo yanayoathiri jamii katika kituo hicho, Afisa wa Mipango wa AMAKENI CBO, Bi Linah Mudhike, amesema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuwapa vijana jukwaa la kujieleza, kujadili changamoto zao, na kuibua suluhisho endelevu zitakazosaidia kuboresha maisha yao.

“Maskani Yetu for Peace inatupa nafasi ya kuwakutanisha vijana kutoka mitaa mbalimbali ya Kisauni, kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya amani, uongozi, na fursa za kiuchumi zinazopatikana. Tunataka kuona vijana wakibadilisha fikra na kuwa nguzo ya maendeleo katika jamii zao,” amesema Mudhike.

Bi Muthike ameongeza kuwa shirika hilo limepanga kushirikiana na wadau mbalimbali wa serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha vijana hao wanapata mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, na stadi za maisha zitakazowawezesha kujitegemea.

Kwa upande wake, Afisa wa Vijana wa Kaunti ya Mombasa kwa maeneo ya Kisauni na Nyali, Bi Rhoda Kisunza, amewataka vijana wengi zaidi kujiunga na maskani hiyo na pia kujisajili katika hazina za vijana zinazotolewa na serikali, ikiwemo Youth Enterprise Development Fund (YEDF).

“Serikali imetoa fursa nyingi za kuwasaidia vijana kujikimu kimaisha. Ninawahimiza kutumia miradi kama hii kama daraja la kupata taarifa, kujifunza, na kujiunga na programu za kifedha zitakazowawezesha kujiajiri badala ya kungoja ajira kutoka kwa serikali,” amesema Kisunza.

Baadhi ya vijana walionufaika na mradi huo wameueleza kuwa ni hatua muhimu inayowapa matumaini mapya na mwelekeo chanya maishani. Wameeleza kuwa kupitia maskani hiyo, sasa wana nafasi ya kushiriki kwenye mijadala ya kijamii, kujifunza mbinu za kibiashara, na kushirikiana katika miradi ya maendeleo.

“Awali tulikuwa hatuna sehemu rasmi ya kukutana na kujadiliana, lakini kupitia Maskani Yetu for Peace tumeweza kupata mwelekeo mpya. Tumejifunza umuhimu wa amani, umoja na kujituma katika kutafuta mafanikio,” amesema mmoja wa vijana walionufaika.

Mradi huu wa Maskani Yetu for Peace unatarajiwa kuenea katika maeneo mengine ya Kaunti ya Mombasa ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira, utovu wa nidhamu, na ongezeko la uhalifu miongoni mwa vijana.

Kwa ujumla, uzinduzi wa kituo hicho umeibua matumaini mapya kwamba vijana wa Kisauni sasa watakuwa kiini cha mabadiliko chanya, wakitumia maskani hiyo kama ngazi ya kujiletea maendeleo na kuchangia ustawi wa jamii zao.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!