Taasisi ya Masoroveya nchini imetaja ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu ardhi kuwa miongoni mwa changamoto kuu zinazoathiri utekelezaji wa mfumo wa usajili wa ardhi kwa njia ya kidijitali, hatua ambayo serikali imekuwa ikihimiza kama njia ya kuongeza uwazi, kupunguza migogoro na kurahisisha utoaji wa hati miliki.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kitaalamu wa masoroveya uliofanyika jijini Nairobi, Rais wa Taasisi hiyo Erick Nyadimo amesema changamoto ya upungufu wa taarifa sahihi imekuwa ikichelewesha utekelezaji kamili wa mfumo wa kidijitali, jambo linalozuia wananchi wengi kupata huduma za ardhi kwa haraka na kwa njia rahisi.
“Ukosefu wa taarifa sahihi na zilizosasishwa kuhusu ardhi unasababisha ucheleweshaji wa upatikanaji wa hati miliki, kuongeza uwezekano wa migogoro ya umiliki, na kudhoofisha juhudi za serikali katika kuimarisha usimamizi wa ardhi. Tunahitaji mfumo wa kidijitali unaoendeshwa kwa data sahihi na zinazoweza kuthibitishwa,” amesema Nyadimo.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kushirikiana kwa karibu na wizara husika pamoja na mashirika ya kimataifa ili kuhakikisha tafiti za kisayansi, upimaji wa kina, na usanifishaji wa ramani za ardhi zinafanyika kwa kutumia teknolojia za kisasa kama vile Geographic Information Systems (GIS) na satellite mapping.
“Kupitia teknolojia hizi, tunaweza kuunda kanzidata ya taifa yenye taarifa zote muhimu za ardhi kwa usahihi mkubwa, jambo litakalorahisisha usajili wa ardhi kwa njia ya kidijitali na kuongeza imani ya wananchi katika mfumo huo,” ameongeza Nyadimo.
Kauli hiyo imeungwa mkono na naibu rais wa taasisi hiyo Nelly Mbugua, ambaye amesisitiza umuhimu wa serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya upimaji na masoroveya, ili kuwezesha wataalamu wa ardhi nchini kutumia teknolojia mpya zinazoboresha ufanisi wa kazi zao.
“Sekta ya masoroveya ni nguzo muhimu katika maendeleo ya ardhi nchini. Serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika mafunzo, vifaa vya kisasa na teknolojia za kidijitali ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa ardhi na kuepuka migogoro inayoibuka mara kwa mara,” amesema Bi. Mbugua.
Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu kwa taasisi za elimu na vyuo vikuu vinavyotoa mafunzo ya masoroveya na uhandisi wa ardhi kuboresha mitaala yao ili iendane na mahitaji ya sasa ya teknolojia na mfumo wa kidijitali.
Kwa upande wao, washiriki wa mkutano huo wamepongeza juhudi za serikali katika kuanzisha mfumo wa usajili wa ardhi kwa njia ya kidijitali, wakisema hatua hiyo itaongeza uwazi na kupunguza mianya ya rushwa katika utoaji wa huduma za ardhi.
Mkutano huo umehudhuriwa na wataalamu wa ardhi, wahandisi, na wawakilishi kutoka sekta binafsi na za umma, ambao walikubaliana kuwa teknolojia ndiyo suluhisho la kudumu katika kuboresha usimamizi wa ardhi na kuongeza tija katika sekta ya ardhi nchini.
NA HARRISON KAZUNGU.