MAMLAKA YA BANDARI YASIFIA UWEKEZAJI ULIOINUA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI NA UTALII.
By Dayo Radio
Published on 29/10/2025 15:20
News

Mamlaka ya Bandari humu nchini imesifia pakubwa mafanikio yake katika kuimarisha huduma za bandari na sekta ya utalii kufuatia juhudi endelevu za uwekezaji unaotekelezwa na wakuu wa mamlaka hiyo.

Akizungumza na wanahabari katika hafla ya mapokezi ya meli ya kifahari SH DIANA mapema leo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Kapteni William Ruto, amesema ujio wa meli hiyo umevunja rekodi ya kihistoria kwa kukaa zaidi ya siku nne nchini. Meli hiyo imebeba zaidi ya watalii 100 na imeshusha abiria katika bandari mbalimbali ikiwemo Bandari Mpya ya Shimoni Kaunti ya Kwale, Bandari ya Lamu na hatimaye Mombasa.

“Ujio wa meli ya SH DIANA ni mafanikio makubwa kwa taifa letu, kwani ni mara ya kwanza meli ya kitalii kukaa kwa muda mrefu nchini na kutua katika bandari zaidi ya moja. Hii inaashiria ukuaji chanya wa sekta ya utalii na uwekezaji katika bandari zetu,” amesema Kapteni Ruto.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari, Bw. Benjamin Tayari, amepongeza mafanikio hayo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukuza sekta ya utalii.

“Tunaona mafanikio haya kama ishara kwamba Kenya imeanza kutambulika kimataifa kama kituo muhimu cha meli za kitalii. Kama mamlaka, tutaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali yanayomiliki meli za abiria ili kuimarisha zaidi sekta hii,” amesema Tayari.

Hata hivyo ameongezakuwa sasa ni wakatiwa serikaliya kitaifa ishurikiane na zile za kanti ili kutufuta soko zaidi zaidi litakalosaidia kukuza sekta ya utalii humu nchini.

“Ni muhimu kwa serikali kuu na serikali za kaunti, hasa zile za ukanda wa Pwani, kutumia mbinu bunifu za kutangaza vivutio vyetu vya utalii katika mataifa ya nje. Tukifanya hivyo, tutaongeza idadi ya watalii na kuchochea ukuaji wa uchumi wetu.”

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!