Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule ametoa wito kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, akisisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za pamoja kukuza uchumi wa kikanda.
Akizungumza mjini Malindi wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Utalii kati ya Uganda na Pwani ya Kenya (Uganda–Kenya Coast Tourism Conference), Chibule amesema ushirikiano wa aina hii ni muhimu katika kuunganisha vivutio vya ndani na vya pwani, hivyo kutoa fursa pana zaidi kwa watalii wa ndani na wa kimataifa.

“Kongamano hili linaonyesha wazi kwamba ushirikiano ni nguzo kuu ya mafanikio katika sekta ya utalii. Tukishirikiana kama eneo la Afrika Mashariki, tunaweza kujenga bidhaa ya utalii yenye mvuto wa kipekee duniani,” amesema Chibule.
Ameongeza kuwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi itaendelea kushirikiana na Serikali ya Kitaifa na nchi jirani katika kuendeleza sera na mikakati inayolenga kukuza utalii endelevu, kuimarisha miundombinu, na kuongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake katika jamii za wenyeji.
“Tunataka kuona jamii zetu zikifaidi moja kwa moja kutokana na utalii. Hii inamaanisha kuweka mazingira bora kwa wawekezaji, kuendeleza ubunifu, na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu za asili zinalindwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” ameongeza.
Chibule pia amewashukuru washirika wote waliounga mkono kongamano hilo, akiwemo Wizara ya Utalii na Wanyamapori, serikali ya Uganda, na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, kwa mchango wao katika kuendeleza ajenda ya kukuza utalii wa kikanda.
Kongamano hili la siku mbili linaendelea mjini Malindi, likiwa na kaulimbiu ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa ajili ya utalii endelevu na jumuishi.
NA HARRISON KAZUNGU.