Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA), Kapteni William K. Ruto, ameahidi kuwa taasisi hiyo itaendelea kuboresha huduma na miundombinu yake ili kuimarisha ufanisi wa sekta ya usafirishaji na biashara barani Afrika.
Akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Biashara na Usafirishaji (International Trade and Logistics Summit - ITLS) lililofanyika jijini Mombasa tarehe 27 Oktoba 2025, Kapteni Ruto aliipongeza Chama cha Wafanyabiashara wa Kenya (KNCCI) na Chama cha Wakala wa Usafirishaji wa Mizigo (KIFWA) kwa kuandaa kongamano hilo muhimu.
“Kongamano hili limekuja kwa wakati muafaka kwani dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji na biashara. Ni muhimu kwa bara la Afrika kukumbatia teknolojia hizi mpya ili kuboresha ufanisi na ushindani katika sekta yetu,” amesema Kapteni Ruto.

Aidha, amebainisha kuwa biashara na usafirishaji ni nguzo kuu za maendeleo ya kiuchumi, hasa katika eneo la Afrika Mashariki.
“Biashara na usafirishaji ndiyo injini ya maendeleo inayounganisha wazalishaji na watumiaji, na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma,” ameongeza.
Kapteni Ruto ametaja miradi mbalimbali ambayo mamlaka ya bandari (KPA) imekuwa ikiitekeleza ili kuongeza uwezo wa bandari na kurahisisha utoaji wa huduma.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa gati la 19B katika Bandari ya Mombasa, mipango ya gati la 23 na 24, pamoja na uendelezaji wa bandari mpya za Lamu na Shimoni na eneo maalum la kiuchumi la Dongo Kundu.
“Tunajivunia kuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya sekta hii. Tumekuwa tukiwekeza katika miundombinu migumu na laini, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kisasa na mifumo ya kiotomatiki inayolenga kuongeza kasi ya kutoa huduma,” amesema.
Akitoa takwimu za utendaji wa Bandari ya Mombasa, kapteni Ruto amesema kuwa kati ya Januari na Septemba 2025, bandari hiyo ilihudumia tani milioni 32.86 za mizigo ikilinganishwa na tani milioni 29.97 mwaka uliopita ongezeko la tani milioni 2.8 sawa na asilimia 9.6. Kiwango cha kontena kiliongezeka kwa asilimia 6.2, kikiwa jumla ya TEUs milioni 1.55.
Wakati uo huo amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano thabiti kati ya KPA na wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara.
“Tunaelewa kuwa jukumu letu si tu kuendesha bandari, bali pia kusaidia kujenga mfumo wa biashara endelevu na jumuishi unaowahusisha wadau wote,” amesema.
Akihitimisha hotuba yake, Kapteni Ruto alitoa wito kwa washiriki wote wa kongamano hilo kushirikiana kwa karibu zaidi na kutumia ubunifu katika kutatua changamoto za sekta. “Tushirikiane, tuvumbue na tuendelee kujifunza ili kuimarisha mustakabali wa biashara na usafirishaji nchini Kenya, barani Afrika na duniani kote,” amehitimisha.
NA HARRISON KAZUNGU.