SERIKALI YAZIDI KUJENGA UUNGWAJI MKONO MLIMA KENYA, YAJIVUNIA MAFANIKIO YA MAENDELEO.
By Dayo Radio
Published on 26/10/2025 08:05
News

Maafisa wakuu wa serikali wamezidisha juhudi za kuwarai wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto, wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza miradi ya maendeleo licha ya malalamiko yanayoendelea kuhusu gharama kubwa ya maisha na ahadi ambazo bado hazijatekelezwa kikamilifu.

Wakati wa kongamano la uhamasishaji wa serikali lililofanyika katika shule ya msingi ya Kahuguini, Gatundu Kusini, maafisa hao wameeleza kuwa miradi mikubwa inayotekelezwa katika eneo hilo imelenga kubadilisha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kikao hicho kimeongozwa na Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura kwa ushirikiano na Waziri wa Ardhi na Makazi Alice Wahome, pamoja na makatibu wakuu akiwemo Salome Beacco (Huduma za Magereza), Mary Muthoni (Afya ya Umma), Alex Wachira (Nishati na Petroli), na Elijah Mwangi (Michezo). Viongozi kadhaa wa mashirika ya serikali pia wamehudhuria.

Waziri Wahome amesema wizara yake imepiga hatua kubwa katika kidigitali cha huduma za ardhi ili kuongeza uwazi na kupunguza ulaghai, akifafanua kuwa utekelezaji kamili wa mpango huo unahitaji takribani shilingi bilioni 35.

“Tumeleta uwazi na ufanisi katika shughuli za ardhi kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa tunashirikiana na wadau kuhakikisha mfumo huu unatekelezwa kote nchini,” amesema Wahome.

Makatibu wakuu Beacco na Muthoni wamewahimiza vijana wa eneo hilo kuepuka matumizi ya dawa za kulevya na pombe, wakisema tabia hizo zimekuwa zikidhoofisha uwezo na mustakabali wa vijana wengi.

Wamewataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na serikali kama Ajira Digital, Makazi Nafuu na mpango wa NYOTA ili kujijengea maisha bora na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Tuna vijana wengi magerezani leo kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na pombe ambazo mara nyingi husababisha uhalifu. Tunawahimiza wajilinde na maovu haya kwa manufaa ya maisha yao ya baadaye,” amesema Beacco.

“Ulevi na matumizi ya mihadarati bado ni changamoto kubwa katika eneo la Mlima Kenya. Ndiyo maana tumeanza ziara za kutoa hamasa kuhusu madhara yake,” ameongeza amesema Muthoni.

Kwa upande wake, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema serikali ya Kenya Kwanza imefanikiwa kutekeleza ahadi nyingi muhimu, akitaja miongoni mwa mafanikio hayo kuwa ni kupungua kwa bei ya mbolea, ajira kwa walimu wapya, na kuundwa kwa nafasi za kazi ndani na nje ya nchi.

“Hakuna serikali iliyowahi kufanya kama hii. Tumeajiri walimu wengi zaidi tangu uhuru, tumepunguza gharama ya mbolea, tumedhibiti uchumi na tumeunda fursa mpya za ajira,” amesema Mwaura.

Juhudi hizi za serikali zimekuja wakati wakazi wa Mlima Kenya wakiendelea kueleza kutoridhishwa kwao na gharama ya juu ya maisha, kiwango kikubwa cha ushuru, na kasi ndogo ya kutimiza baadhi ya ahadi za kampeni.

Eneo la Mlima Kenya linabaki kuwa ngome muhimu kisiasa kwa Rais Ruto, ambaye anajitahidi kuimarisha uungwaji mkono wake katika eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!