NAIBU GAVANA WA KILIFI FLORA MBETSA CHIBULE AWATAKA MAAFISA WA UTENDAJI KUONGOZA KWA UADILIFU NA UWAZI.
By Dayo Radio
Published on 23/10/2025 20:19
News

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule amewataka Maafisa wa utawala wa kaunti ndogo na wadi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya uongozi bora, uwazi na uadilifu, ili kuhakikisha huduma bora na maendeleo endelevu kwa wananchi katika ngazi za mashinani.

Akizungumza katika mafunzo ya utangulizi yanayoendelea kwa siku tatu katika eneo la Mnarani, Kaunti ya Kilifi, Bi. Chibule amesisitiza kuwa Maafisa wa utawala ni nguzo muhimu katika mfumo wa ugatuzi, kwa kuwa wao ndio moyo wa utoaji huduma mashinani na kiungo cha moja kwa moja kati ya serikali na wananchi.

Hata hivyo ameeleza kuwa mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na idara ya utumishi wa umma, utawala, mawasiliano na maendeleo shirikishi kwa ushirikiano na Shirika la WWF, yana lengo la kuimarisha uwezo wa viongozi hao katika uongozi, uratibu, mawasiliano na uwajibikaji, ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za serikali kwa wananchi.

“Nawahimiza viongozi wetu wa utawala kuongoza kwa uadilifu, haki na uwazi. Ni muhimu washirikiane kwa karibu na idara mbalimbali za serikali ya kaunti, wafanye kazi kwa moyo wa kujitolea, na waweke maslahi ya wananchi mbele ya maslahi binafsi. Uongozi unaomweka mwananchi katikati ya maendeleo ndio msingi wa mafanikio yetu,” amesema Bi Chibule.

Amesisitiza zaidi kuwa viongozi hao wanapaswa kuzingatia ushirikiano, umoja na nidhamu kazini, huku wakihakikisha kwamba vijana na wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

“Tunataka kuona viongozi wanaochochea mabadiliko chanya katika jamii. Viongozi wanaosikiliza wananchi, wanaowasaidia kupata suluhisho la changamoto zao, na wanaoleta matumaini mapya kwa vizazi vijavyo,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Naibu Gavana, Serikali ya mstahiki gavana Gideon Maitha Mung’aro imejikita katika kujenga utawala shirikishi na unaowajibika, unaolenga kutoa huduma zenye ubora na matokeo halisi kwa wananchi wote wa Kaunti ya Kilifi bila upendeleo.

Amebainisha kuwa chini ya uongozi wa Gavana Mung’aro, serikali ya kaunti inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utumishi wa umma na kuhakikisha kila idara inatekeleza wajibu wake ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.

“Tunataka kuona Kaunti ya Kilifi ikiongozwa kwa misingi ya uwazi, maadili na uadilifu. Serikali hii inathamini sana mchango wa maafisa wa utawala kwa kuwa wao ndio daraja linalounganisha mipango ya serikali na uhalisia wa maisha ya wananchi. Tukishirikiana, tunaweza kufanikisha malengo ya maendeleo na kuinua ustawi wa jamii zetu,” amesisitiza.

Aidha amehitimisha kwa kusema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa serikali wa kujenga uwezo wa watumishi wa umma, ili wawe na ujuzi, maadili na uongozi unaozingatia utumishi kwa wananchi, uwajibikaji na maendeleo jumuishi.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!