SERIKALI YAONYA WATU WANAOENEZA LUGHA ZA CHUKI WAKATI WA MAOMBOLEZO YA TAIFA.
By Dayo Radio
Published on 23/10/2025 13:11
News

Serikali imeonya vikali wanasiasa na viongozi wa umma wanaotoa matamshi ya chuki na uchochezi katika kipindi hiki cha maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha kiongozi wa upinzani Raila Amollo Odinga, akisisitiza kuwa taifa linahitaji umoja, si migawanyiko.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Msemaji wa Serikali, Seneta Dkt. Isaac Mwaura, amesema kauli zilizotolewa na Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga, ni za kusikitisha, hazina uzalendo na hazistahili kutolewa wakati taifa linaomboleza kifo cha kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika siasa na demokrasia ya Kenya.

"Ni jambo la kusikitisha na lisilokubalika kabisa kuona baadhi ya viongozi wakitumia kipindi hiki cha huzuni kueneza maneno ya chuki yanayoweza kugawa Wakenya. Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote anayevunja sheria kwa kutoa matamshi ya uchochezi," amesema Dkt. Mwaura.

Ameeleza kuwa serikali ya Rais Dkt. William Ruto inatilia mkazo usawa wa mgao wa rasilimali za kitaifa, na kwamba hakuna sehemu yoyote ya nchi imeachwa nyuma. Amewataka viongozi kuacha kutumia siasa za kikanda na kijamii kueneza propaganda zinazoleta migawanyiko miongoni mwa wananchi.

"Serikali hii imeweka msingi wa usawa katika ugawaji wa rasilimali na maendeleo. Hakuna kaunti inayopendelewa, kila sehemu inapata haki yake kulingana na mipango ya kitaifa. Hivyo, ni busara kwa viongozi kuhubiri umoja badala ya kugawanya taifa," amesema Mwaura.

Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki cha maombolezo, viongozi wanapaswa kuwa mfano wa amani na mshikamano, wakizingatia kuwa marehemu Raila Odinga alikuwa kiongozi aliyepigania haki, uwazi, na umoja wa Wakenya.

"Kumbukumbu ya marehemu Raila Odinga inapaswa kutuunganisha, si kutugawa. Alikuwa kiongozi aliyeamini katika haki, usawa, na Kenya moja. Ni wakati wetu sasa kuheshimu urithi wake kwa kulinda amani na umoja wa taifa letu," ameongeza.

Aidha, serikali imekaribisha uamuzi wa Gavana Mutahi Kahiga kujiuzulu kama Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), ikisema huo ni mfano wa uwajibikaji wa kisiasa unaopaswa kuigwa na viongozi wengine. Wakati huo huo, serikali imezitaka taasisi za Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Maridhiano (NCIC) na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayepatikana akieneza chuki, kwa mujibu wa sheria za nchi.

"Hatutaruhusu mtu yeyote kuharibu amani ya nchi hii kwa maneno ya uchochezi. Sheria ipo wazi, na taasisi zetu za ulinzi na usalama zitachukua hatua mara moja kwa yeyote anayevunja sheria kwa kueneza chuki," alionya Mwaura.

Serikali imesisitiza kuwa kipindi hiki cha maombolezo kinapaswa kuwa wakati wa kutafakari, kuombea familia ya marehemu na kuenzi mchango wake kwa taifa. Dkt. Mwaura amewataka Wakenya wote kuwa wavumilivu, kuheshimiana na kuendeleza maono ya amani, demokrasia na umoja ambayo marehemu Raila Odinga aliyasimamia kwa maisha yake yote ya kisiasa.

"Tuungane kama taifa kumuenzi kiongozi huyu kwa kudumisha maadili aliyoyapigania  umoja, uadilifu na Kenya yenye matumaini kwa wote," amesema Mwaura akihitimisha taarifa yake.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!