Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Mipango ya Kitaifa, (CPA) Kuria Kimani, amewaomba wakenya kutumia kikamilifu njia za kidijitali zilizowekwa na serikali ili kunufaika na mifumo ya uwekezaji na hifadhi ya pensheni itakayowasaidia kujipanga vyema kwa maisha ya uzeeni.
Akiwahutubia wanahabari mapema leo katika Kongamano la Zamara Pension Convention 2025 lililofanyika katika mjini Mombasa, Kimani amesema kuwa serikali imewekeza katika mifumo ya kidijitali inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za fedha na uwekezaji, ili kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wao wa kifedha.
Kimani amesema kuwa ni wajibu wa kila mkenya kuanza kuwekeza mapema ili kujihakikishia maisha bora na yenye heshima baada ya kustaafu.
“Ni muhimu kila mmoja wetu aanze kufikiria kesho leo. Uwekezaji wa kidijitali si suala la anasa, bali ni nyenzo muhimu ya kujitayarisha kwa maisha ya baadaye. Tusiwe kizazi kinachotegemea bahati, bali kizazi kinachopanga na kuwekeza kwa hekima.”amesema Kuria Kimani
Aidha ameongeza kuwa mifumo ya kisasa ya kidijitali imeleta uwazi, ufanisi na urahisi wa upatikanaji wa huduma, na hivyo kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya pensheni.
“Teknolojia imebadilisha jinsi tunavyofanya mambo. Hatuwezi kuendelea kutumia mbinu za zamani katika dunia inayoendelea kubadilika kwa kasi. Ni lazima tuunganishe nguvu, sekta binafsi na umma, ili kuhakikisha hakuna Mkenya anayesalia nyuma katika safari ya maandalizi ya kustaafu,” alisema Kimani.
Kaulimbiu ya kongamano hilo, “Disrupting for Impact: Transform, Integrate, and Sustain”, imesisitiza umuhimu wa mageuzi ya kiteknolojia na ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujenga ustawi wa kifedha unaojumuisha Wakenya wote.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya Jamii (RBA), Charles Machira, amesema serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha sekta ya pensheni inabaki thabiti, ikiwemo kuhamasisha umma kuhusu faida za kuwa wanachama wa mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii.
“Tunataka kuona kila Mkenya, iwe ni mfanyakazi wa ofisini au mjasiriamali mdogo, ananufaika na mpango wa pensheni. Hii ndiyo njia pekee ya kujenga jamii yenye usalama wa kifedha.”
Hata hivyo afisa Mtendaji Mkuu wa Zamara Group, Sundeep Raichura, amesisitiza umuhimu wa ubunifu na ujumuishaji wa teknolojia katika sekta ya pensheni, akieleza kuwa mustakabali wa sekta hiyo unategemea uwezo wa wadau kuhimili mabadiliko ya kidijitali.
“Tunapaswa kubadilika na kuhimiza uwekezaji unaoleta athari chanya. Hii itatupa jamii yenye nguvu na wananchi walio tayari kwa maisha baada ya kazi,” amesema Raichura.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau wa sekta ya fedha, waajiri, wachambuzi wa uchumi, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na washikadau wa mifuko ya pensheni kutoka Kenya na Afrika Mashariki. Lengo kuu limekuwa ni kuhamasisha utamaduni wa uwekezaji endelevu, kuongeza uelewa wa hifadhi ya jamii, na kuhimiza maandalizi ya maisha bora baada ya kustaafu kwa kutumia teknolojia za kisasa.
NA HARRISON KAZUNGU.