Idara ya Upelelezi DCI imeanzisha msako kumtafuta mwombolezaji aliye nyakua bunduki ya mlinzi wa Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, wakati wa mazishi ya marehemu Raila Amolo Odinga mjini Bondo, Siaya.
Kulingana na ripoti ya polisi, tukio hilo lilitokea majira ya saa kumi na nusu jioni Jumapili, nje ya chuo cha JOOUST, wakati kundi la vijana waliokuwa wakifanya fujo liliizingira gari la Gavana.
Katika mkwaruzano na msongamano wa waombolezaji hao, bastola ya Konstebo Benson Olayo, iliyokuwa na risasi kumi na tano ,ilinyakuliwa na mshukiwa ambaye alitorokea kwenye umati wa waombolezaji.
Polisi wamesema kwamba wingi wa watu eneo hilo uliathiri juhudi za kumkamata mshukiwa mara moja huku DCI wakianzisha uchunguzi na kutoa wito kwa umma kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kurejesha silaha hiyo.
Tukio hili limeibua wasiwasi kuhusu usalama wa viongozi katika hafla kubwa za hadhara.