MWENYEKITI WA LAPSET ALI MENZA MBOGO ATOA WITO WA KUHESHIMU UGATUZI NA KUACHA SIASA ZA UKUBILA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MASHUJAA.
By Dayo Radio
Published on 20/10/2025 19:05
News

Mwenyekiti wa Bodi ya Mradi wa Lamu Port-South Sudan-Ethiopia Transport (LAPSET), Ali Menza Mbogo, amewataka Wakenya kuenzi, kulinda na kuutumia vyema mfumo wa ugatuzi, akisema kuwa ni moja ya urithi mkubwa uliowachwa na mwendazake Raila Amollo Odinga, aliyekuwa waziri mkuu wa zamani na kinara wa chama cha ODM.

Akizungumza mapema leo katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Mashujaa iliyofanyika katika wadi ya Magogoni, eneobunge la Kisauni, Kaunti ya Mombasa, Mbogo amewataka wananchi kuzingatia misingi ya ugatuzi kama chombo cha maendeleo na usawa wa kiuchumi katika ngazi za kaunti. 

Aidha amesema kuwa kupitia ugatuzi, maeneo yaliyokuwa yamesahaulika kwa miaka mingi yamepata fursa ya kuimarika na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Ugatuzi ni matokeo ya mapambano marefu ya mashujaa wetu waliotaka kila Mkenya ahisi nguvu na manufaa ya serikali katika eneo lake. Ni wajibu wetu kulinda msingi huo, kuutumia ipasavyo na kuhakikisha unaendelezwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” amesema Mbogo huku akipongezwa na umati wa wakazi waliohudhuria hafla hiyo.

Mbogo amewataka viongozi wa kisiasa kuiga mfano wa viongozi waliotangulia kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya kutanguliza ubinafsi na misimamo ya kisiasa inayogawa jamii. 

Katika kauli yenye uzito, amemkashifu vikali Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali, akimtaka aache mara moja kuendeleza siasa za ukubila na chuki ambazo, kwa mujibu wake, zinahatarisha amani na mshikamano wa wakazi wa Mombasa.

“Siasa za kugawanya watu kwa misingi ya koo, dini au rangi hazina nafasi katika taifa linalotaka kusonga mbele. Tunapaswa kuwa kitu kimoja, tukijenga Mombasa na Kenya yenye umoja na ustawi,” amesisitiza Mbogo.

Mbogo pia amewataka vijana kote nchini kujitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura ili kutumia sauti yao kuchagua viongozi wanaoleta maendeleo, uwajibikaji na matumaini. Alisema kuwa vijana ndio nguzo kuu ya taifa na wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mwelekeo wa siasa nchini endapo watatumia kura zao kwa busara.

“Vijana msiwe watazamaji katika safari ya maendeleo. Jisajilini, shiriki kwenye maamuzi na hakikisheni mnapigia kura viongozi wanaojali wananchi, si wale wanaotafuta vyeo kwa maneno matupu,” amehimiza Mbogo.

Akihitimisha hotuba yake, Mbogo aliwakumbusha wananchi kuenzi mashujaa wote waliotoa maisha yao katika kupigania uhuru, haki na demokrasia nchini, akisema kuwa mashujaa wa kweli ni wale wanaoendelea kuhimiza amani, umoja na maendeleo kwa wote.

Hafla hiyo ya mashujaa imehudhuriwa na viongozi wa kidini, wazee wa mitaa, vijana na kina mama, waliotumia nafasi hiyo kumpongeza Mbogo kwa uongozi wake wa busara na misimamo yake ya kuhimiza umoja na maendeleo katika Kaunti ya Mombasa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!