VIJANA WA WADI YA BOFU WATOA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA RAILA ODINGA
By Dayo Radio
Published on 19/10/2025 06:17
News

Huku taifa zima likiendelea kugubikwa na majonzi kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani na kinara wa chama cha ODM, Raila Amolo Odinga, hisia za huzuni na majonzi zimeendelea kutanda kote nchini. Katika wadi ya Bofu, eneobunge la Likoni kaunti ya Mombasa, vijana wamejitokeza kwa wingi kutoa rambirambi zao na kumkumbuka marehemu kama nguzo muhimu ya siasa na umoja wa taifa la Kenya.

Vijana hao, wakiongozwa na Murshid Muhammad Athman, ambaye pia ni mkereketwa wa masuala ya kisiasa na kijamii, wamesema kifo cha Raila Odinga ni pigo kubwa si kwa chama cha ODM pekee, bali kwa taifa lote la Kenya.

 

Vijana hao wameeleza kuwa mwendazake kama kiongozi aliyejitolea kwa moyo wa dhati kupigania haki, demokrasia, na usawa kwa wananchi wote.

“Baba Raila alikuwa mtu wa watu, aliyetanguliza amani na umoja wa taifa letu. Alijitolea kupigania haki na maendeleo ya kila Mkenya bila ubaguzi,” amesema Murshid Muhammad Athman, huku akionekana mwenye huzuni kubwa.

Murshid ameendelea kueleza kuwa Raila Odinga aliweka msingi thabiti wa demokrasia ya kweli nchini na alikuwa mlezi wa wengi katika siasa huku akihimiza vijana kuiga mfano wake wa uongozi wa uadilifu, uvumilivu na uthabiti.

“Baba alikuwa mwanga wa matumaini kwa vijana wengi. Alitufundisha kuwa siasa ni chombo cha kuleta mabadiliko chanya, si uhasama. Ni jukumu letu sasa kuendeleza maono yake ya Kenya yenye umoja, haki na maendeleo,” ameongeza Murshid.

Kauli yake iliungwa mkono na Bi Ngare, mmoja wa vijana waliohudhuria kikao hicho cha kuomboleza, ambaye amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani wakati huu wa majonzi.

“Tunawaomba Wakenya waomboleze kwa utulivu na umoja, kwani Baba alikuwa kiongozi wa amani na upendo. Kupitia kwake tulipata mfumo wa ugatuzi ambao umeleta huduma karibu na wananchi, na sasa kila Mkenya anahisi kuguswa na serikali,” amesema Bi Ngare.

Bi Ngare aidha ameongeza kuwa mchango wa Raila katika kuleta mageuzi ya kikatiba na kisiasa hautasahaulika, akisisitiza kuwa kizazi kipya kina jukumu la kuhakikisha urithi wake wa uongozi unaendelezwa.

“Ni jukumu la viongozi wa ODM kuendeleza urithi wa Raila wa kuunganisha taifa na kutetea haki za wananchi. Tunawaomba wasiruhusu chama kipoteze mwelekeo wake wa msingi wa umoja na haki,” ameongeza Bi Ngare.

Vijana hao pia walitumia fursa hiyo kuwahimiza wanasiasa wa kizazi kipya kutanguliza maslahi ya wananchi kuliko ya kibinafsi, wakisema huo ndio ujumbe mkuu aliouacha Raila Odinga kwa taifa la Kenya.

“Raila alikuwa kiongozi aliyetamani kuona vijana wakijitokeza kushika nafasi za uongozi. Alituamini, na sasa ni wakati wetu kuonyesha dunia kwamba maono yake hayakufa naye,” amehitimisha Murshid Muhammad Athman.

Kwa sasa, vijana wa Bofu wamepanga kufanya ibada maalum ya kumbukumbu na maombi, wakisema wataendelea kushirikiana na viongozi wa chama cha ODM katika kuendeleza miradi ya kijamii na kuimarisha umoja miongoni mwa wananchi kama njia ya kumuenzi marehemu Raila Amolo Odinga.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!