SERIKALI YATANGAZA SIKU YA MAPUMZIKO KUMUENZI MAREHEMU RAILA ODINGA
By Dayo Radio
Published on 16/10/2025 07:56
News

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, ametangaza Ijumaa, tarehe kumi na saba Oktoba mwaka huu wa 2025, kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa kwa heshima ya Waziri Mkuu wa zamani, marehemu Raila Amollo Odinga, aliyefariki dunia akiwa nchini India alipokuwa akipokea matibabu.

 

Kupitia Gazeti Rasmi la Serikali , Waziri Murkomen amesema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa Wakenya wote kumuenzi kiongozi huyo mkongwe ambaye alihudumia taifa kwa muda mrefu.

 

Ibada ya mazishi ya kitaifa inatarajiwa kufanyika Ijumaa hii katika Uwanja wa Nyayo kuanzia saa mbili asubuhi, ikihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wageni wa kimataifa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

 

Baada ya ibada hiyo, mwili wa marehemu utaelekezwa nyumbani kwake Karen kwa mkesha wa maombi, kisha kusafirishwa siku ya Jumamosi kuelekea Kisumu na hatimaye Bondo, Kaunti ya Siaya, ambako mazishi yatafanyika siku ya Jumapili, tarehe kumi na tisa Oktoba.

 

Bendera kote nchini zinaendelea kupepea nusu mlingoti hadi siku ya mazishi, huku vitabu vya rambirambi vikiendelea kuwekwa katika ofisi za serikali, balozi na ofisi za chama cha ODM.

Comments
Comment sent successfully!