VIJANA PWANI KUNUFAIKA NA USHIRIKIANO MPYA KATI YA TVET NA KEPSA.
By Dayo Radio
Published on 14/10/2025 17:49
News

Ni afueni kwa vijana kote nchini, hususan wale wa ukanda wa Pwani, baada ya Taasisi ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) kuingia katika ushirikiano wa kimkakati na Muungano wa Waajiri wa Sekta Binafsi Nchini (KEPSA) ili kuboresha mfumo wa utoaji wa elimu ya kiufundi, uhalisia wa vyeti, na kuongeza fursa za ajira kwa wahitimu.Akizungumza jijini Mombasa wakati wa hafla ya kuzindua rasmi ushirikiano huo, Kaimu Katibu wa TVET, Bw. Joseph Njau, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana wengi wanaohitimu kutoka vyuo vya kiufundi, ikiwemo ukosefu wa ajira, utoaji wa vyeti visivyotambulika, na kukosa muunganiko na sekta ya ajira.

“Tumeamua kushirikiana na KEPSA kwa sababu tunatambua kuwa sekta binafsi ndio injini kuu ya ajira nchini. Tunataka kuhakikisha kuwa vijana wanaohitimu kutoka vyuo vyetu vya TVET wanakuwa tayari kuingia sokoni, wakiwa na ujuzi, maarifa, na vyeti vinavyotambulika na waajiri. Hii itasaidia kupunguza idadi ya vijana wasio na ajira,” amesema Bw. Njau.

Alifafanua kuwa ushirikiano huo utahusisha utekelezaji wa programu za mafunzo kwa vitendo (industrial attachments) kwa wanafunzi wa TVET katika kampuni na taasisi zinazohusishwa na KEPSA, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata uzoefu wa moja kwa moja wa kazini kabla ya kuhitimu.

Aidha, kupitia makubaliano hayo, KEPSA itasaidia TVET katika kubuni mitaala ya mafunzo inayolenga mahitaji halisi ya soko la ajira. Kwa mujibu wa Bw. Njau, hatua hiyo itahakikisha kuwa kile kinachofundishwa darasani kinahusiana moja kwa moja na kile kinachohitajika na waajiri.

“Tunataka kuondoa ule pengo kati ya elimu na ajira. Kwa muda mrefu, tumekuwa na changamoto ambapo vijana wanahitimu lakini wanakosa kazi kwa sababu ujuzi walioupata hauendani na mahitaji ya sekta. Kupitia ushirikiano huu, tutahakikisha mitaala yetu inahuishwa mara kwa mara kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko,” ameongeza.

Bw. Njau pia alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika malezi ya kisaikolojia na kitaaluma kwa vijana wanaosoma katika vyuo vya kiufundi, akisema kuwa mpango huo pia unalenga kutoa ushauri nasaha na mwongozo wa kitaaluma kwa wanafunzi ili kuwajengea imani, nidhamu na uelewa wa fursa zilizopo katika sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu, zaidi ya vijana 350,000 hujiunga na vyuo vya kiufundi kila mwaka nchini Kenya, huku idadi kubwa ikiwa ni kutoka kaunti za Pwani kama vile Kilifi, Kwale, Mombasa, Taita Taveta, na Lamu. Hata hivyo, wengi wao wamekuwa wakikosa ajira rasmi kutokana na ukosefu wa uhusiano thabiti kati ya taasisi za elimu na sekta ya ajira.

Ushirikiano huu mpya kati ya TVET na KEPSA unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu ya kiufundi kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu anakuwa na cheti kinachotambulika, ujuzi unaohitajika sokoni, na fursa ya kupata ajira au kujiajiri.

Mpango huu utaanza kutekelezwa rasmi kuanzia mwaka ujao katika vyuo mbalimbali vya TVET kote nchini, huku serikali ikiahidi kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya vyuo, vifaa vya mafunzo, na ushirikiano na sekta binafsi ili kukuza uchumi kupitia vijana wenye ujuzi.

“Huu sio mwanzo wa makaratasi, bali mwanzo wa mabadiliko halisi katika elimu ya kiufundi nchini. Tunataka kila kijana atambue kuwa elimu ya ufundi ni nguzo ya maendeleo, sio chaguo la mwisho,” amehitimisha Bw. Njau kwa matumaini makubwa.

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!