Kenya imeshuhudia idadi kubwa zaidi ya watalii mwaka 2024 ikilinganishwa na miaka iliyopita; ni kauli ya Waziri wa Utalii, Bi. Rebecca Miano.Akizungumza katika Kongamano la Utalii Ukanda wa Pwani, Bi. Miano alisema: “Kenya ilisajili idadi kubwa ya watalii mwaka jana na sasa tunatarajia idadi hiyo kufikia milioni 5.5 mwishoni mwa mwaka 2028.”
Aidha, alibainisha mipango ya serikali ya kuimarisha sekta hiyo.
“Serikali inalenga kupanua usafiri wa anga ukanda wa Pwani pamoja na kuboresha miundomsingi mingine katika sekta hii ili kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” alisema Waziri Miano.
Akizungumzia umuhimu wa sekta ya utalii, Waziri huyo aliongeza: “Sekta ya utalii imekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa huku ikisajili jumla ya shilingi bilioni 452.20 katika kipindi cha mwaka 2024–2025, kiwango ambacho wadau wa sekta hii wanaazimia kuongeza mwaka huu.”
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Kilifi, Bi. Flora Mbetsa Chibule, alisema.
“Ukanda wa Pwani ni uti wa mgongo wa sekta ya utalii nchini hali ambayo imechangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi kwa taifa.”

Pia aliwahimiza vijana kuzingatia nafasi zinazotokana na sekta hiyo.
“Sekta ya utalii imebuni nafasi nyingi za ajira kwa vijana na nawahimiza wazikumbatie ili wajiendeleze kimaisha,” amesema Bi. Chibule.