Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Bi. Flora Mbetsa Chibule, amewarai wakaazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kushiriki ipasavyo katika demokrasia ya nchi.
Akizungumza na wanahabari mapema leo, Bi. Chibule alisema.
“Ni haki ya kila mmoja kujihusisha katika masuala ya upigaji kura, hususani vijana, ili kuepukana na migogoro inayotokea baada ya uchaguzi.”
Aidha, alisisitiza umuhimu wa mshikiano kutoka kwa Tume ya Uchaguzi (IEBC) katika kusaidia makundi maalum. “Naomba maafisa wa IEBC wawe mstari wa mbele kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanashiriki bila kizuizi chochote katika usajili huu,” alisema.
Kuhusu masuala ya kibinadamu, hasa ugavi wa chakula eneo la Ganze, Bi. Chibule alitoa wito kwa wanasiasa kutoweka siasa katika changamoto za wananchi.
“Ni vyema tuache kuingiza siasa katika suala la ugavi wa chakula Ganze, bali tutumie mbinu zinazofaa kusuluhisha changamoto zinazowakabili wakazi wa eneo hilo,” amesema.
Pia, aliwatia moyo wananchi kushirikiana katika kuimarisha amani na mshikikano wa kijamii.
“Tukishirikiana kama jamii moja, tunaweza kupata suluhisho la changamoto zetu bila kutegemea siasa za mgawanyiko,” amesema Bi. Chibule.