SIKU YA AMANI DUNIANI – KISAUNI, MOMBASA
By Dayo Radio
Published on 27/09/2025 21:52
News

Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani katika Kaunti ya Mombasa yameadhimishwa katika Eneo Bunge la Kisauni, Wadi ya Shanzu.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo kundi kubwa la Wana-Bodaboda ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakihusishwa na visa vya uhalifu.

Hata hivyo, jamii pamoja na viongozi wa kiserikali wamewashukuru Wana-Bodaboda kwa juhudi zao za kuimarisha usalama katika maeneo yao ya kazi na makaazi.

Akiongoza hafla hiyo, Bi. Akinyi Pamela ambaye ndiye Naibu Kamishna wa Kaunti, Tarafa ya Bamburi, amewataka wakazi wote wa Mombasa hususan wa Kisauni kudumisha amani. Aidha, amewaonya viongozi wa kisiasa na wa kidini waache kuwatia hofu wafuasi wao kwa kuwashawishi kwamba mahasimu wao wako karibu nao. Amesisitiza kuwa yeyote atakayepotosha amani atakabiliwa ipasavyo na Serikali.

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kama vile Bamburi Charity Network, KECOSCE, Dream Achievers Youth Organization, na Epic Youth Organization yameungana pamoja kufanikisha siku hii muhimu, nao pia wakahimiza wito huohuo wa kudumishwa kwa amani.

Kwa upande wao, Wana-Bodaboda waliapa kuendeleza usalama kazini kwao na kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria zilizoidhinishwa na Serikali.

 

By Rajab Juma

Comments
Comment sent successfully!