BALOZI WA SOMALIA AOMBA RADHI KUFUATIA UDHALILISHAJI WA BENDERA YA KENYA .
By Dayo Radio
Published on 26/09/2025 10:06
News

Balozi wa Somalia nchini Kenya, Jabril Ibrahim Abdulle, ameomba radhi rasmi kufuatia tukio la udhalilishaji wa bendera ya Kenya katika uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi, wakati wa mechi ya mchujo ya Kombe la Klabu Bingwa Barani Afrika kati ya Mogadishu City FC na Kenya Police FC.

Tukio hilo lilihusisha baadhi ya mashabiki wa Mogadishu City FC, waliorekodiwa wakidhalilisha bendera ya taifa kwa kuitemea mate na kuikanyaga kitendo kilichozua hisia kali miongoni mwa Wakenya.

Kupitia taarifa rasmi, klabu ya Mogadishu City FC imejitenga na matendo hayo, ikiyataja kuwa ya aibu, yasiyokubalika, na kinyume kabisa na maadili ya michezo. Klabu hiyo pia iliomba msamaha kwa serikali ya Kenya na wananchi wake kwa kile ilichokiita kitendo kisichoakisi msimamo wala mwenendo wa timu hiyo na mashabiki wake kwa ujumla.

Tukio hilo limeibua ghadhabu kutoka kwa Wakenya wengi, huku viongozi wa kisiasa, wanaharakati wa kijamii, na mashirika ya kiraia wakitoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika ili kulinda heshima ya taifa na kudumisha nidhamu katika mashindano ya kimataifa.

Comments
Comment sent successfully!