AGA KHAN HOSPITAL YAADHIMISHA SIKU YA SARATANI YA AKINA MAMA DUNIANI
By Dayo Radio
Published on 20/09/2025 19:46
News

Aga Khan Hospital Mombasa imeadhimisha World Gynecologic Oncology Day kwa kushirikiana na washikadau mbalimbali wa afya katika juhudi za kupambana na saratani za akina mama.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari shughuli hii imeungwa mkono na kupigwa jeki na mradi wa East Africa Comprehensive Women Cancer Project (EACwCP) unaotekelezwa na Aga Khan Hospital Mombasa kwa ufadhili wa AfD, Gates Foundation na Aga Khan Foundation (AKF).

Kwa mujibu wa Aquinius Mungatia, Meneja wa Mradi Aga Khan Hospital Mombasa, mradi huu unalenga kuboresha miundombinu ya huduma za saratani ili kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa huduma za kina kwa wagonjwa katika hospitali zinazoshirikishwai na katika jamii. 

Aidha, mradi huu unajikita katika kujenga uwezo wa wahudumu wa afya kupitia mafunzo, kuongeza ujuzi wa kitaaluma, kuimarisha huduma za kinga kwa jamii hususan uchunguzi wa mapema, na kukuza tafiti za pamoja ili kuwezesha mbinu bora za matibabu.

"Kupitia mradi huu, tunalenga kuokoa maisha kwa kuhakikisha wanawake wanapata uchunguzi wa mapema na matibabu ya saratani kwa gharama nafuu. Tunataka kuona jamii ikiwa na matumaini mapya kupitia huduma bora na endelevu za afya," amesema Mungatia.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), saratani ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani, huku saratani za akina mama kama saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zikichangia kwa kiwango kikubwa. Nchini Kenya, takribani visa vipya 42,000 vya saratani vinaripotiwa kila mwaka na zaidi ya vifo 27,000 vinatokana na ugonjwa huu. Saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi ndizo zinazoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake, huku ukosefu wa uchunguzi wa mapema na gharama za matibabu zikitajwa kama changamoto kubwa.

Mradi huu unalenga wakaazi wa Kaunti za Mombasa na Kilifi ambapo unatarajiwa kuwanufaisha takribani watu milioni 1.8.

Hata hivyo hatua hii inalenga kuendana na mikakati ya kitaifa ya kudhibiti saratani kwa kuimarisha huduma endelevu zinazojumuisha uchunguzi wa mapema, matibabu, ufuatiliaji na usaidizi kwa waathirika.

Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Aga Khan Hospital Mombasa imetangaza kupunguza gharama za vipimo vya uchunguzi wa saratani hadi mwishoni mwa Novemba 2025 katika hospitali kuu na vituo vyake 18 vya afya vilivyoko ukanda wa Pwani.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!