RAIS RUTO AZINDUA HUDUMA YA TRENI YA ABIRIA MJINI MOMBASA
By Dayo Radio
Published on 17/09/2025 13:39
News

Rais William Ruto ameongoza uzinduzi rasmi wa huduma ya Mombasa Commuter Rail Service leo, Septemba 17, 2025, mjini Mombasa.

Huduma hiyo inalenga kuondoa msongamano wa magari, kupunguza ajali na gharama za usafiri, huku ikirahisisha safari kati ya katikati ya jiji la Mombasa na kituo cha reli cha SGR Miritini. 

Treni hiyo itapita vituo vya Miritini, Changamwe Magharibi, Changamwe Mashariki, Shimanzi, Mazeras na Mombasa CBD, na itabebeba zaidi ya abiria 4,000 kusafiri kwa urahisi kila siku.

Rais Ruto aidha amesema mradi huu ni hatua ya kihistoria kwani unafufua umuhimu wa kilomita zero, eneo ambapo reli ya Kenya–Uganda ilianzia zaidi ya miaka 130 iliyopita.

 “Kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwa SGR mwaka 2017, abiria wanaweza kuanza safari zao moja kwa moja kutoka jiji la Mombasa,” amesema Rais.

Aliongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupanua mtandao wa reli nchini hadi Malaba kupitia Kisumu, na pia kuunganisha na Ukanda wa LAPSSET, ili kukuza usafiri salama, wa kisasa na endelevu.

Kwa kutangaza huduma hiyo rasmi kuwa imeanza kazi, Rais Ruto amesisitiza kuwa reli hii mpya si tu suluhisho la usafiri, bali ni alama ya historia ya Kenya, na ahadi ya mustakabali bora.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!