GAVANA ABDULSWAMAD NASSIR AKARIBISHA KAMATI YA MAANDALIZI YA ODM AT 20 JIJINI MOMBASA
By Dayo Radio
Published on 14/09/2025 10:37
News

 Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amekaribisha rasmi Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Miaka 20 ya ODM (ODM at 20 Planning Committee) mjini Mombasa, hatua inayoashiria hamasa kubwa kuelekea maadhimisho makuu ya chama hicho.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 12 mjini Mombasa, ikiwaleta pamoja viongozi wa chama, wanachama na wafuasi kutoka pembe zote za nchi.

Akizungumza baada ya kikao na kamati hiyo, Gavana Nassir amesema kuwa kaunti ya Mombasa imejipanga vilivyo kutumia siku hiyo ili kueka uhusiano dhabiti baina ya viongozi wa chama hicho na hata wafuasi wake.

"Mombasa iko tayari kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya ya kihistoria. Tumepiga hatua kubwa katika maandalizi na tunawahakikishia wanachama wote wa ODM na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kwamba tutawakaribisha kwa heshima na taadhima.”

Aidha amesema kuwa siku hiyo pia itatumika kuziba mapengo ya chama hicho ili kuleta sura mpya kwa wakenya.

"Sherehe hizi hazitakuwa tu za kusherehekea miaka 20 ya chama chetu, bali pia ni fursa ya kutafakari safari tuliyopitia na kuweka dira ya kisiasa kwa siku zijazo.”

Hata hivyo ODM inatarajiwa kutumia jukwaa hilo kusherehekea mafanikio yake ya kisiasa, kuimarisha mshikamano wa wanachama wake na pia kuweka mikakati ya mustakabali wake wa kisiasa.

Shughuli hiyo imeanza kuibua hamasa kubwa miongoni mwa wafuasi wa ODM na inatazamiwa kuvutia maelfu ya wageni jijini Mombasa.

 

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!