ISK YALAANI MAUAJI YA WAKILI KYALO MBOBU NA KUWEPO KWA VITENDO VYA VURUGU VINAVYOHUSIANA NA BODABODA.
By Dayo Radio
Published on 12/09/2025 20:45
News

Chama cha masoroveya humu nchini (Institution of Surveyors of Kenya – ISK) kimetuma risala za rambirambi kwa famili na wa wakenya kwa ujumla kufuatia mauaji ya kikatili ya wakili mashuhuri wa mahakama Kuu ya Kenya, Bw. Kyalo Mbobu, yaliyotokea jioni ya tarehe 9 Septemba 2025.

Ikitoa taarifa kwa vyombo vya habari ISK imetoa pole zake za dhati kwa familia, marafiki na pia chama cha mawakili wa humu nchini(LSK), ikisema tukio hili ni tishio la usalama nchini linalochochewa na matumizi mabaya ya pikipiki.

Katika taarifa hiyo ISK imesisitiza kuwa kutokana na kifo hicho ipo haja ya haraka ya kushughulikia tatizo la uhalifu unaotumia bodaboda, ambalo limewagharimu wakenya maisha.

Hata hivyo chama hicho kimelaani vikali vitendo vya madereva wa bodaboda ambao mara nyingi huchukua sheria mikononi baada ya ajali na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na kueneza hofu miongoni mwa watumiaji wa barabara mbalimbali humu nchini.

Kwa mujibu wa ISK, tatizo hili linaonyesha pengo kubwa katika udhibiti na uwajibikaji ndani ya sekta ya bodaboda, hali inayowapa nafasi wahalifu kutumia pikipiki kutekeleza uhalifu kisha kutoroka haraka.

Kwa msingi huo, ISK imetoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za dharura, ikiwemo:

Kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji ya Bw. Kyalo Mbobu na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.

Kufanya mageuzi ya usajili na utambulisho wa pikipiki, kwa mfano kuweka namba kubwa na zinazosomeka kwa urahisi kama ilivyo Rwanda.

Kudhibiti kwa ukali sekta ya bodaboda kupitia usimamizi thabiti, vyama vilivyo na mpangilio na utekelezaji wa sheria za barabarani.

Kuweka mikakati ya kuhakikisha ulinzi wa wananchi na wataalamu wote ili kuzuia vitendo vya vurugu na hofu.

Inspekta Jenerali wa Polisi kufanya uchunguzi wa haraka na kuwaleta waalifu wa vurugu zinazohusiana na pikipiki kulingana na sheria.

ISK imesema Kenya haiwezi kuendelea kupoteza maisha na mali kwa mikono ya wahalifu wanaojificha kwenye mwavuli wa usafiri wa bodaboda. 

Chama hicho aidha kimeitaka serikali, watunga sera na viongozi wa sekta ya bodaboda kulitazama suala hili kama kipaumbele cha kitaifa.

“Maisha ya wananchi lazima yawekwe mbele ya yote,” imesema ISK, ikiongeza kuwa imesimama pamoja na familia ya marehemu Bw. Mbobu, wanasheria na Wakenya wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa udhibiti wa sekta ya bodaboda.

NA HARRISON KAZUNGU.

Comments
Comment sent successfully!