VIONGOZI WA KIDINI PWANI WALAANI MATUMIZI YA MIHADARATI
By Dayo Radio
Published on 09/09/2025 16:48
News

Muungano wa viongozi wa kidini(Patriotic Religious Leaders) ukiongozwa na Sheikh Abu Qatada, ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo umeibuka na msimamo mkali dhidi ya matumizi ya mihadarati ambayo yameendelea kuwa kero kubwa kwa vijana katika ukanda huo.

Wakizungumza katika kikao cha pamoja, viongozi hao walieleza kuwa dawa za kulevya zimegeuka kuwa chanzo kikuu cha kuporomoka kwa maisha ya vijana, kusambaratisha familia na kulemaza maendeleo ya kijamii na kiuchumi. 

Sheikh Abu Qatada amesema wazi kuwa tatizo hilo limevuka kiwango cha kawaida na linahitaji mshikamano wa dhati kati ya serikali, jamii na viongozi wa kidini.

“Mihadarati imeporomosha maisha ya vijana wetu, imegawanya familia na kuacha maumivu makubwa katika jamii. Hatutakaa kimya tukiona hali hii ikiendelea,” Sheikh Abu Qatada alisema kwa kusisitiza.

Aidha, viongozi hao wametaja nafasi ya dini katika mapambano hayo kuwa ya msingi, wakihimiza serikali kushirikiana kwa karibu na taasisi za kidini kuandaa programu za uhamasishaji na mafunzo yanayoweza kuwasaidia vijana kuacha dawa za kulevya. 

“Dini ni nguzo ya maadili. Kupitia mafundisho yake tunaweza kuwavuta vijana waliokwama kwenye mihadarati na kuwarudisha kwenye njia ya haki,” ameongeza Sheikh Abu Qatada.

Muungano huo pia ulitoa wito kwa wazazi na walezi kuhusika kikamilifu katika malezi ya vijana kwa kushirikiana na viongozi wa kidini. 

Aidha viongozi hao wamesema malezi ya kimaadili na kiroho yakiwa na mshikamano wa kijamii ni silaha madhubuti ya kuwanusuru vijana.

 “Wazazi wasiwakabidhi tu serikali jukumu la malezi. Jamii nzima inapaswa kushirikiana na dini ili kuokoa vijana wetu,” wameongeza viongozi hao.

Kwa mujibu wa Patriotic Religious Leaders, iwapo jamii, serikali na viongozi wa dini watashirikiana kwa dhati, tatizo la mihadarati litapungua kwa kiwango kikubwa na kizazi cha sasa kitapata mwanga wa matumaini na maisha bora ya baadaye.

Comments
Comment sent successfully!