Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir, ametangaza rasmi uzinduzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Biashara na Usafirishaji wa 2025 (International Trade & Logistics Summit – ITLS 2025) utakaofanyika tarehe 27–28 Oktoba mjini Mombasa.
Mkutano huu utawaleta pamoja viongozi wa sekta ya biashara na usafirishaji kutoka mataifa mbalimbali, serikali, wawekezaji na wavumbuzi kwa lengo la kujadili mustakabali wa biashara, bandari, teknolojia ya usafirishaji na usimamizi wa minyororo ya usambazaji barani Afrika Mashariki na kwingineko.
ITLS 2025 utajikita katika mada kuu zikiwemo matumizi ya teknolojia katika huduma za usafirishaji, uendelevu kupitia bandari za kijani, ushirikiano wa mipakani na mageuzi ya kidigitali yanayolenga kuharakisha biashara. Hatua hii inaiweka Mombasa katikati ya mazungumzo ya kimataifa kuhusu biashara na usafirishaji.
“Mombasa ina nafasi ya kipekee kijiografia katika Bahari ya Hindi na maono makubwa ya kujenga uchumi wa kisasa na endelevu. Tunajivunia kuwa lango kuu la Afrika Mashariki na Kati na tunakaribisha dunia kuwekeza, kuvumbua na kushirikiana nasi,” alisema Gavana Nassir.
Mkutano huu unatarajiwa kuimarisha nafasi ya Mombasa kama kitovu cha biashara na fursa, huku wageni kutoka mataifa mbalimbali wakitarajiwa kuhudhuria.
NA HARRISON KAZUNGU.