Ni afueni kubwa kwa wafanyabiashara wadogowadogo katika Kaunti ya Mombasa kufuatia ujio wa mpango mpya wa benki ya Equity unaolenga kuwawezesha kupata mikopo ya kuinua biashara zao. Benki hiyo imezindua rasmi tawi jipya katika eneo la Kengeleni, hatua inayolenga kuimarisha huduma kwa wateja na kukuza maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya mtaa na viunga vyake.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, mkurugenzi wa tawi hilo, Nassir Abdallah, ameeleza kuwa mpango huo unalenga kutoa suluhisho la kifedha kwa wafanyabiashara wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi.

“Lengo na madhumuni ya kuanzisha tawi hili ni kuhakikisha wafanyabiashara wadogowadogo wanapata mikopo nafuu itakayowasaidia kuinua biashara zao, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi,” amesema Nassir Abdallah.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa waendesha bodaboda katika Kaunti ya Mombasa, Samuel Ogutu, amesema kuwa mpango wa mikopo hiyo umeleta mwanga mpya kwa vijana wengi katika sekta hiyo.
“Ujio wa mikopo hii umetusaidia pakubwa. Tumeweza kuinua sekta ya bodaboda na wengi wetu sasa tunajivunia maisha bora,” amesema Samuel Ogutu.
Aidha ameongeza kuwa ushirikiano kati yao na benki hiyo unapaswa kuungwa mkono ili kufanikisha maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla.
NA HARRISON KAZUNGU.