Mamlaka ya bandari humu nchini imechukua hatua muhimu katika kuboresha na kuleta ufanisi katika michakato ya ununuzi kwa kuzindua rasmi mfumo wa ununuzi serikalini kwa njia ya kielektroniki (E-GP). Serikali ilianzisha mfumo huo kamili wa kielektroniki tarehe 1 Julai 2025, na kuagiza kuwa shughuli zote za ununuzi wa bidhaa, ikiwemo zile za chini ya mikataba ya mfumo wa utekelezaji wa pamoja zifanyike kupitia jukwaa hilo.
Hatua hii inalenga kurahisisha taratibu za ununuzi, kupunguza utaratibu wa kutumia karatasi na kukuza uwazi zaidi katika taasisi zote za serikali.

Akizungumza mapema leo katika Chuo cha Bandari cha Maritime Academy wakati wa mafunzo kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) kuhusu mfumo huo, Mkurugenzi Mkuu Capt. William Ruto amesisitiza umuhimu wa kukumbatia teknolojia ili kuboresha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa kiutendaji.
“Mfumo huu wa E-GP ni hatua ya mageuzi inayotuweka sambamba na dira ya taifa ya kuwa na sekta ya umma ya kisasa, inayowajibika, na yenye ufanisi,” amesema Capt. Ruto.
Mafunzo hayo yanayoendeshwa na maafisa kutoka hazina ya kitaifa ni sehemu ya mpango mpana wa kujenga uwezo ambao utawafikia wakurugenzi wakuu na wasimamizi waandamizi wa KPA huku ikiwa lengo ni kuwawezesha wahusika katika manunuzi na usimamizi wa ugavi kupata ujuzi wa kutumia mfumo huo wa kidijitali kwa ufanisi.
Mkurugenzi mkuu huyo aidha ameeleza vipengele muhimu vya mfumo huo, ambavyo vinalenga kuleta mabadiliko ya kiteknolojia kwenye ununuzi, kwa kufanya michakato iwe wazi na ya gharama nafuu.
Utekelezaji wa E-GP utajumuisha maeneo mbalimbali kama vile usajili wa wasambazaji kwa njia ya mtandao, mipango ya ununuzi ya kila mwaka kwa njia ya mtandao, zabuni za kielektroniki, minada ya kielektroniki, usimamizi wa mikataba kidijitali, udhibiti wa huduma nyenginezo kwa njia za kidijitali na malipo ya kielektroniki.
“Utekelezaji wa mfumo wa E-GP hautaboresha tu ufanisi wetu wa kiutendaji, bali pia utaimarisha uaminifu na uadilifu katika usimamizi wa rasilimali za umma. Mfumo huu utarahisisha mzunguko wa manunuzi, kuboresha usimamizi wa data, na kuhakikisha kufuata viwango vya kitaifa,” ameongeza Capt. Ruto.
Hata hivyo amewataka wafanyakazi kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kukumbatia mabadiliko hayo kwa ari na moyo wa kujitolea.
“Dhamira na ushirikiano wenu ni muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya jukwaa hili. Kwa pamoja, tutajenga Mamlaka ya Bandari ya kisasa inayokidhi mahitaji ya siku za usoni,”
Utekelezaji wa mfumo wa E-GP unatarajiwa kuiweka KPA katika nafasi ya kuigwa katika ununuzi wa sekta ya umma, na hivyo kuchangia kufanikisha malengo mapana ya maendeleo ya taifa ambapo mfumo huu unalingana na azma ya serikali ya kuwa na huduma ya umma yenye uwazi, ufanisi na inayojibu mahitaji ya wananchi.
NA HARRISON KAZUNGU.