Jumlya wabunge 304 Jumanne waliupigia kura mswada unaolenga kuhalalisha kikatiba hazina tatu watakazosimamia kwa lengo la kujifaidi.
Bunge la Kitaifa ambalo nyakati fulani hukosa idadi tosha ya wabunge linaposhughulikia miswada ya kufaidi wananchi liliandikisha historia kwa kuvutia idadi kubwa zaidi ya wabunge walioungana kupitisha mswada huo wa marekebisho ya Katiba.
Aidha, wabunge wa ODM walijasirika kwenda kinyume na msimamo wa kiongozi wao Raila Odinga na kupiga kura ya kuunga mkono mswada huo.
Mswada huo wa Marekebisho ya Katiba ya 2025, unalenga kuhalalisha kikatiba, Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF), Hazina ya Usawazishaji (NGAAF) na Hazina ya Seneti kuhusu Ufutiliaji wa Utendakazi wa Serikali za Kaunti (SOF).
Ingawa sheria ya NG-CDF haiwaruhusu wabunge kusimamia matumizi ya fedha za hazina hiyo, wana usemi katika utoaji wa zabuni kwa miradi inayofadhiliwa na fedha za hazina hiyo. Shughuli hiyo huzongwa na ufisadi na wizi wa fedha za umma inavyofichuliwa kila mwaka kwenye ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kuna visa ambapo kampuni zinazomilikiwa na wabunge ndizo hupewa zabuni za kutekeleza miradi inayofadhiliwa kwa pesa za NG-CDF.