Mwenyekiti wa kutathmini utendakazi wa polisi (IPOA) Isaac Hassan amefika mbele ya Kamati ya Bunge ya Usalama na kutoa ushahidi kuhusu uchunguzi unaoendelea wa kifo cha mwanablogu maarufu wa masuala ya kijamii na siasa Albert Ojwang.
Katika kikao hicho Hassan amethibitisha kuwa Ojwang alifariki dunia akiwa kizuizini katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi na kufichua kwamba kanda za CCTV za kituo hicho ziliweza kuhujumiwa kwa lengo la kupoteza ushahidi wa tukio hilo.
Pamoja na hayo mwenyekiti huyo wa IPOA amesisitiza kwamba tume yake itaendelea na uchunguzi wa kina na huru ili kuhakikisha haki inatendeka kwa familia ya marehemu
“Tunahakikisha serikali na umma wa Wakenya kwamba hakuna atakayelindwa. Wote waliohusika katika kifo cha Albert Ojwang watachukuliwa hatua stahiki mara tu uchunguzi utakapokamilika"
Kifo cha Albert Ojwang kimeendelea kuzua mijadala mikali na maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi huku wanaharakati, familia na mashirika ya kutetea haki za binadamu wakishinikiza haki kutendeka na wahusika kuwajibishwa.
Tume ya IPOA imekuwa ikiongoza uchunguzi huo kwa kushirikiana na idara nyingine za uchunguzi wa jinai, huku maafisa watano wa polisi wakitajwa kama washukiwa wa awali na kuondolewa kwenye majukumu yao wakati uchunguzi ukiendelea.
Mazishi ya Ojwang yanatarajiwa kufanyika wiki ijayo katika kaunti ya Homa Bay.