Wadau wa sekta ya afya wamezitaka serikali za kaunti, ya Kilifi na Mombasa, kuongeza bajeti ili kuboresha huduma za afya ya uzazi na kuwawezesha watu wanaoishi na ulemavu kupata huduma bora za afya na bima ya afya kwa wote
Wakizungumza mjini Kilifi Jumatano, Juni 11, 2025, mashirika ya vijana ya Dream Achievers na Stretchers, yanayotekeleza mradi wa We Lead, yamesisitiza umuhimu wa juhudi endelevu katika kulinda haki za watu wenye ulemavu na kuboresha huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango
Afisa wa mradi huo, Bi. Sophie Pwani, ameeleza kuwa utekelezaji wa We Lead ni hatua muhimu inayosaidia kufanikisha sheria, sera na mazoea yanayolinda haki za wanawake vijana.

“We Lead ni mpango wa kina unaowajengea uwezo wasichana na wanawake vijana kuwa watetezi wa haki zao kwa kuwapa msaada wa kuendesha harakati za utetezi wa maana na endelevu kuhusu afya na haki zao za uzazi.”
Aidha ametoa wito kwa serikali za kaunti kuhakikisha kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kuna mgao maalum wa fedha kwa ajili ya huduma za ukarabati, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, na kuwawezesha walezi wa watoto wenye ulemavu.
“Tunazitaka kaunti zitenge fedha zaidi kwa huduma za ukarabati na kuhakikisha kuna mistari ya bajeti mahsusi kwa ajili ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, ili kuepuka kuwabagua au kuwaweka kando.”
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Idara ya Jinsia na Huduma za Jamii wa Kaunti ya Kilifi, Fredric Nguma, amesema kuwa serikali ya kaunti hiyo imejumuisha masuala ya ulemavu, wanawake, vijana na afya ya uzazi katika bajeti ya mwaka 2025/2026.

“Katika Kaunti ya Kilifi, ambapo wasichana na wanawake, wakiwemo wenye ulemavu, wameathirika na mimba zisizotarajiwa na ukatili wa kijinsia, tumeweka mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na DAYO na mashirika mengine. Tunaona kupungua kwa visa vya mimba za mapema kutokana na jitihada hizi. Hatutalegeza kamba kwa sababu hili ni jukumu letu.”
Afisa wa mradi wa Stretchers Youth Organization, Mary Wasike, ameonyesha jinsi mradi huo umelenga kuimarisha ushawishi wa wanawake wanaokumbwa na changamoto mbalimbali, wakiwemo wanaoishi na virusi vya HIV, watu wenye ulemavu, waliotawanywa na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

“Katika miaka mitano iliyopita, tumebuni maeneo salama na shirikishi ambapo wasichana na wanawake wamepata nafasi ya kuzungumza wazi, kuongoza na kutetea haki zao katika jamii, mashuleni na kwingineko. Tumeshuhudia wakivunja vizingiti, wakikabiliana na unyanyapaa na kuleta mabadiliko halisi.”
Mradi wa We Lead unatekelezwa katika nchi tisa barani Afrika, Asia na Amerika: Lebanon, Jordan, Niger, Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda, Guatemala na Honduras. Katika nchi hizi, wanawake na vijana kutoka makundi manne watu wenye ulemavu, wanaoishi na HIV, waliotawanywa na wanaoishi katika mazingira magumu ndio walengwa wakuu.

Nchini Kenya, shirika la Dream Achievers Youth Organization (DAYO) na Stretchers ni kati ya mashirika 12 ya jamii yanayoongozwa au yanayohudumia makundi haya ya walengwa katika kaunti mbalimbali, kwa lengo la kuboresha haki za afya ya uzazi kwa vijana.