Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Johnson Sakaja, ameeleza masikitiko yake kufuatia kifo cha Albert Ojwang’ kilichotokea akiwa chini ya ulinzi katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi mnamo Juni 8, 2025. Akiwahutubia wanachama wa Muungano wa Waendelezaji Mali (KPDA) katika jumba la City Hall, Nairobi, tarehe 19 Machi 2025, Gavana Sakaja alitoa ahadi ya kuisimamia familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.
“Nimemfahamu Albert kwa muda mrefu. Ukiangalia mitandao yake ya kijamii kama Facebook na Twitter, utaona alikuwa mshawishi wa watu binafsi. Tutasimama na familia yake katika safari hii. Tutagharamia mazishi, kumsomesha mwanawe George Miles mwenye umri wa miaka mitatu, na kumalizia ada ya chuo ya mjane wake,” alisema Gavana Sakaja.

Aidha, alimhakikishia mjane wa Ojwang’ kwamba atakapokamilisha masomo yake ya afya katika muhula wa mwisho, ataajiriwa katika serikali ya kaunti ili aweze kujikimu pamoja na mwanawe.
“Tutahakikisha anapata ajira mara tu atakapomaliza mafunzo yake ya afya, kwani yuko katika muhula wa mwisho wa masomo,” aliongeza Sakaja.
Msaada huo haukuishia kwa mjane na mtoto pekee. Gavana pia aliahidi kuwasaidia wazazi wa marehemu kwa kununua shamba katika Kaunti ya Homa Bay na kuwajengea nyumba za kupangisha ili waweze kujipatia kipato.

Akitambua mchango mkubwa wa Wakenya walioungana kuiunga mkono familia ya Ojwang’, Gavana Sakaja alifichua kuwa michango yote iliyokusanywa itawekezwa katika hazina ya soko la fedha (money market fund) kwa lengo la kuhakikisha usalama wa kifedha wa mtoto wake katika siku zijazo badala ya kutumia pesa hizo zote katika shughuli ya mazishi.
Wakenya wengi walijitokeza kuisaidia familia hiyo baada ya baba wa marehemu kufichua kuwa alimtegemea sana mwanawe ambaye sasa amepoteza maisha.
Akizungumzia kifo hicho cha kusikitisha, Sakaja alilaani vikali mauaji hayo na kusema kuwa taifa haliwezi kuendelea kushuhudia vifo vinavyowaacha watoto bila wazazi.
Gavana Sakaja pia alikutana na baba wa marehemu Albert Ojwang’ katika City Hall mnamo Juni 11, 2025, ambapo alimhakikishia kuwa serikali ya kaunti itasimama na familia yao.
Kifo cha Ojwang’ kimezua maandamano makubwa na wito wa haki kutoka kwa wananchi, wanaharakati na viongozi wanaotaka uwajibikaji kutoka kwa vyombo vya usalama.