Shirika la Dream Achievers Youth Organization (DAYO) limeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa dhima ya kukuza ajenda za vijana na kulinda haki za watu wanaoishi na ulemavu (PWDs).
Katika kuonyesha mshikamano na DAYO, wadau wa jinsia na vijana walitoa ahadi ya kushirikiana na serikali za kaunti ili kuendeleza masuala ya vijana na maendeleo ya kijamii.
Akizungumza wakati wa Gala Dinner ya Maadhimisho ya Miaka 20 yaliyofanyika jijini Mombasa, Afisa wa Jinsia wa Kaunti ya Kilifi, Bi Ruth Dama Masha, alisema kuwa programu za malezi chanya zinazolenga kupunguza mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia (SGBV) ni muhimu katika kukomesha maovu hayo katika jamii.

Mratibu wa Programu wa DAYO, Enos Opiyo, alisema kuwa shirika hilo linaendelea kujenga madaraja baina ya jamii ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kama vile ukosefu wa haki za kijamii, elimu bora, usawa katika huduma za afya, uendelevu wa mazingira na usawa wa kijinsia.
“Unapowajengea uwezo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, unawasaidia kujitegemea kiuchumi, na hivyo kuwakinga dhidi ya ukatili wa kijinsia. Hili ndilo lengo kuu la programu zetu nyingi na tunajivunia kusema tumefanikisha,” alisema Opiyo.

Afisa Mkuu wa Idara ya Vijana, Jinsia, Michezo na Huduma za Kijamii wa Kaunti ya Mombasa, Khamis Juma Kurichwa, alihimiza DAYO kuendelea kuimarisha ushirikiano na mashirika mengine ili kupata msaada zaidi kutoka kwa serikali za kaunti na serikali kuu.
Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka kaunti za Mombasa, Kilifi, Kisumu na Nairobi – maeneo ambayo DAYO imetekeleza miradi yenye athari chanya kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuendeleza maisha na kuchochea maendeleo ya jamii.
Mkurugenzi Mkuu na Mwanzilishi wa DAYO, Seif Jira, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka 20, shirika hilo limekuwa likiwawezesha vijana, kutimiza ndoto zao na kujenga mustakabali bora kwa kushirikiana na washirika waliounga mkono maono yao.
“Kila mtu binafsi, mwanajamii, shirika mshirika, na taasisi ya serikali iliyoandamana nasi, kutuunga mkono na kutetea lengo letu – ASANTENI. Hii ni sherehe ya mafanikio yenu kama ilivyo yetu. Tazameni mbele, kwa miaka mingi zaidi ya athari na ushirikiano!” alisema Jira.

Sherehe hiyo pia iliashiria kufungwa rasmi kwa Mradi wa WEZESHA, uliodhaminiwa na Aga Khan Foundation na kutekelezwa katika kaunti za Mombasa na Kilifi kwa lengo la kukomesha ukatili wa kijinsia na kutetea haki za jamii zilizotengwa.
Kupitia ushirikiano na walimu, polisi, viongozi wa wanawake, wahudumu wa afya, na maafisa wa afya ya jamii mashinani, DAYO ilianzisha kampeni chanya dhidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo hayo.
Vitendo vya ubakaji, ulawiti, na unyanyasaji ni baadhi ya ukatili unaokiuka haki za manusura wengi. Viongozi wa DAYO sasa wanatoa wito kwa mamlaka ya mahakama, waendesha mashtaka, na wanajamii kushirikiana kumaliza kabisa uovu huo.
Kupitia Mradi wa WEZESHA, shirika liliwapa mafunzo ya kina "gatekeepers" kama walimu, wahudumu wa afya, viongozi wa wanawake na wahamasishaji wa afya ya jamii, ili wawe mstari wa mbele katika mapambano haya.
Kwa mujibu wa mratibu wa mradi, Susan Lankisa, juhudi hizi za mara kwa mara zimeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa rufaa za kesi zinazohusu haki za afya ya uzazi (SRHR) na ukatili wa kijinsia (GBV)