Mwenyekiti mteule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Erastus Ethekon Edung na makamishna sita wa tume hiyo wataingia afisini mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu endapo bunge la kitaifa litaidhinisba uteuzi wao.Hii ni baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kuagiza Kamati ya Bunge kuhusu Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) kuanzisha taratibu za kuwapiga msasa saba hao na kuwasilisha ripoti yake bungeni mnamo Mei 27, 2025.
“Ikizingatiwa kuwa shughuli ya kuundwa upya kwa IEBC ni ya dharura, kamati hiyo inatarajiwa kuanza mara moja shughuli ya upigaji msasa na kuwasilisha ripoti yake siku ambayo Bunge la Kitaifa litarejelea vikao vyake mnamo Jumanne, Mei 27, 2025. Hii inaliwezesha bunge kuchambua ripoti hiyo ndani ya wakati uliowekwa kisheria,” akasema Jumamosi alipowasilisha majina ya wateule hao kwa JLAC.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya IEBC ya 2024, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka George Murugara inayo muda wa siku 28 kuendesha vikao vya kuwapiga msasa Bw Edung na wenzake kisha kuwasilisha ripoti katika bunge la kitaifa.
Aidha, bunge hilo limepewa muda wa siku saba kuchambua ripoti hiyo kwa ajili ya kukubaliana na mapendekezo yake au kuyakataa.
Agizo la Spika Wetang’ula kwa kamati ya JLAC linajiri siku mbili baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Rais William Ruto Ijumaa wiki jana na siku moja baada ya kumpendekeza Bw Edung kuwa mwenyekiti wa IEBC.