Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Sheriff Nassir, ameikosoa serikali ya kitaifa kwa madai ya kuzuia fedha muhimu zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, hali ambayo amesema inachangia kusambaratika kwa miundomsingi ya kaunti kutokana na uhaba wa fedha.
Kwa mujibu wa Gavana huyo maafisa walioko Nairobi hawana uelewa wa kina kuhusu mahitaji halisi ya wananchi mashinani, licha ya kudhibiti mabilioni ya fedha zilizotengwa kwa miradi ya barabara.
Haya yanajiri huku kukiwa na mvutano kati ya Rais William Ruto na magavana kuhusu usimamizi wa mfuko wa ukarabati wa barabara (RMLF). Rais Ruto amependekeza kwamba fedha hizo ziendelee kusimamiwa na serikali ya kitaifa na kutumwa moja kwa moja kwa taasisi husika, badala ya kupelekwa kwa serikali za kaunti.
Aidha, Gavana Nassir ameonyesha hofu kuhusiana na hali mbaya ya barabara zilizoharibiwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali za nchi, akisema hali hiyo inachangiwa pia na mfumo duni wa upitishaji majitaka.
Vile vile, amedokeza kuwa mara nyingi magavana hulalamikiwa kuhusu hali duni ya barabara katika maeneo yao, ilhali jukumu la ukarabati wa barabara hizo liko mikononi mwa mashirika ya kitaifa kama vile Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini (KENHA) na Mamlaka ya Barabara za Mijini na Vijijini (KURA).