Published on 12/03/2025 by Dayo Radio
MDHIBITI wa Bajeti, Margaret Nyakang’o, ameonya kuwa shughuli za ofisi yake huenda zikakwama kufuatia kupunguzwa kwa bajeti yake kwa Sh850 milioni katika mwaka ujao wa kifedha Hatua hii inajiri wakati ambapo Dkt Nyakang’o ameanika maafisa wa serikali ya kitaifa kwa kukwepa makusudi mfumo uliowekwa ili kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za walipa kodi.
Bi Nyakang’o alisema kwamba licha ya kuwepo kwa mfumo wa kidijitali ambao unafanya kazi kikamilifu, wizara, idara na mashirika ya serikali bado zinaendelea kufanya maombi ya matumizi ya fedha nje ya mfumo huo, huku wakitumia mfumo huo kwa nadra na kwa uchaguzi mara kwa mara.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti jana, Mdhibiti wa Bajeti alisema kuwa Sh704.25 milioni ambazo ofisi yake ilipokea kwa mwaka wa sasa wa kifedha zimeisha.
Aliambia kamati inayoongozwa na Seneta wa Mandera, Ali Roba, kwamba kwa sasa wanategemea kupata fedha kutoka kwa bajeti ya pili ya nyongeza ili waweze kufanikisha shughuli zao hadi mwisho wa mwaka wa kifedha.
Dkt Nyakang’o alisema kuwa shughuli muhimu kama vile ufuatiliaji na tathmini, utayarishaji wa ripoti, kujenga uwezo, mijadala ya utekelezaji wa bajeti na safari za ndani za kikazi zimekwama baada ya bajeti yao kuisha.
Alifafanua kuwa ufuatiliaji na tathmini, ambao ulikuwa na bajeti ya Sh28.9 milioni, tayari umekwama, sawa na uhamasishaji wa umma na safari za ndani za kikazi.
“Tuna bajeti ndogo sana na tunaendelea tu kwa sababu tumepunguza matumizi yetu hadi kiwango cha chini kabisa,” alisema Dkt Nyakang’o.
Aliongeza kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika mwaka wa kifedha unaoishia Juni 2026, kwani Serikali ya Kitaifa imetenga kiasi cha Sh777.5 milioni pekee kwa ofisi yake, licha ya wao kuomba Sh1.63 bilioni.
Alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizomo kwenye taarifa ya sera ya bajeti, ofisi yake itakumbwa na upungufu wa Sh855.96 milioni.
Dkt Nyakang’o alieleza kuwa kupunguzwa kwa bajeti kutanyima ofisi yake fedha za kutosha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.Alibainisha kuwa maeneo tisa ya kipaumbele katika utendakazi wake yamekumbwa na upungufu wa Sh579.3 milioni, jambo ambalo linaashiria changamoto kubwa kwa ofisi yake.
“Tumetengewa chini ya asilimia 50 ya kile tulichoomba, na itakuwa kazi ngumu kufanikisha malengo yetu,” alisema Dkt Nyakang’o.
“Tunaiomba Seneti iingilie kati na kututengea angalau Sh579.3 zaidi milioni katika mwaka ujao wa kifedha ili kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi. Bila ufadhili huu, tuko kama gari lililokwama,” aliongeza.