Amerika imezima ufadhili wa kima cha dola 13 milioni (Sh1.7 bilioni) kwa kikosi cha walinda usalama kutoka mataifa mbalimbali (MSM), kikiongozwa na Kenya, kinachoendesha operesheni za kurejesha amani Haiti, Umoja wa Mataifa ulithibitisha Jumanne.
Hii ni kufuatia amri ya Rais Donald Trump kwamba Amerika ikatize misaada ya kigeni kwa miezi 90 “kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusu manufaa ya mipango hiyo.”
“Amerika ilikuwa imeahidi kutoa dola milioni 15 (Sh1.95 bilioni), dola 1.7 milioni (Sh22 milioni) kati ya hizo zilikuwa zimetumwa kwa hazina maalum ya UN kwa ufadhili wa shughuli za kupambana na wahalifu Haiti, kwa hivyo dola 13.3 milioni (Sh1.729 bilioni) sasa zimezuiwa,” msemaji wa UN Stephane Dujarric aliwaambia wanahabari.
“Tumepokea ilani rasmi kutoka Amerika kwamba mchango wao umesitishwa,” akaongeza.
Kikosi cha walinda usalama, kinachoshirikisha polisi 627 wa Kenya, kilitumwa Haiti mwaka jana kusaidiana na polisi wa nchi hiyo kurejesha amani kwa kupambana na magenge ya uhalifu. Kutumwa kwa walinda usalama hao kuliidhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa (UNSC) mnamo Oktoba 2023, japo hicho sicho kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Kwa hivyo, ufadhili wa walinda usalama hao unategemea michango ya hiari kutoka mataifa mbalimbali ya ulimwengu, ambayo umekuwa finyu.
NA: HARRISON KAZUNGU