Kashfa kubwa za ufisadi nchini zinapangwa na kutekelezwa na wataalamu wa sekta mbali mbali hii ni kulingana na Tume ya kupambana na Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imefichua.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Dkt David Oginde, alisikitika kuwa wataalamu wamekuwa wakichangia pakubwa katika kufanikisha ufisadi jambo ambalo alisema ni hatari kwa nchi.
“Tumetambua kuwa kashfa nyingi kubwa nchini ni zinazopangwa na kutekelezwa na wataalamu – wasanifu wa majengo, wahandisi, wanasheria, wahasibu, maafisa wa ununuzi, wasimamizi wa wafanyakazi, madaktari miongoni mwa wengine.
Tunataka kuwahimiza waache kutumia utaalamu wao kuwezesha wizi wa fedha za umma. Zaidi ya hayo, mashirika ya kitaaluma yanapaswa kuchukua hatua madhubuti za kutekeleza kanuni zao za maadili ili kukuza maadili mema miongoni mwa wanachama wao,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa EACC amewahimiza viongozi wa kidini kukemea ufisadi katika mahubiri yao na kutekeleza jukumu lao kama walinzi wa maadili katika jamii.
NA HARRISON KAZUNGU.