Wizara ya Kilimo, kwa ushirikiano na serikali za kaunti pamoja na Benki ya Dunia, imeweka mikakati ya kubuni sera na mipango itakayowahamasisha vijana nchini kujitosa katika kilimo cha kisasa na kukifanya kuwa chanzo cha ajira na biashara.
Mikakati hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa chakula nchini, kuimarisha sekta ya kilimo na wakati huo huo kupanua fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana, ambao ni sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini.
Akizungumza mjini Mombasa, Waziri wa Kilimo na Mifugo Mutahi Kagwe amesema serikali inalenga kutumia teknolojia za kisasa pamoja na akili unde katika kilimo ili kubadilisha mtazamo wa vijana kuhusu sekta hiyo na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uzalishaji wa chakula na biashara ya kilimo.
Kagwe amesema matumizi ya teknolojia yatawezesha wakulima kupata taarifa muhimu kuhusu uzalishaji, masoko, hali ya hewa na mbinu bora za kilimo, hatua ambayo amesema itasaidia kuongeza tija na kufanya kilimo kuwa biashara yenye faida zaidi.
“Serikali inalenga kutumia teknolojia na akili unde katika kilimo ili kuwavutia vijana na kuwawezesha kujipatia ajira kupitia kilimo na biashara,” amesema Kagwe.
Waziri huyo amesema serikali pia inaendelea kutafuta njia za kupunguza gharama zinazowakabili wakulima na wawekezaji katika sekta ya kilimo. Kagwe amesema atashirikiana na Hazina ya Taifa kuhakikisha ushuru katika sekta hiyo unapunguzwa ili kuhamasisha uwekezaji na kuwezesha wafanyabiashara na wakulima kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa chakula.
“Tutashirikiana na Hazina ya Taifa kupunguza ushuru katika sekta ya kilimo kwa sababu hatua hiyo itasaidia kuvutia uwekezaji zaidi na kuchochea ukuaji wa sekta hii,” amesema Kagwe.
Aidha, serikali imeeleza kuwa ushirikiano na serikali za kaunti pamoja na washirika wa maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, utasaidia kuhakikisha sera na mipango inayowekwa inazingatia mahitaji halisi ya vijana na wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakati huo huo, Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya kilimo nchini, amewataka vijana kuwa makini na kutotumiwa vibaya kisiasa, hasa wakati taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Lusaka amesema vijana wanapaswa kutumia muda na nguvu zao kujenga maisha yao kupitia fursa za kiuchumi badala ya kuruhusu kutumiwa katika shughuli za kisiasa zinazoweza kuwanyima nafasi ya kujenga maisha bora.
“Vijana wasikubali kutumiwa vibaya kisiasa. Siasa ni za muda, lakini kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi,” amesema Lusaka.
Amehimiza vijana kukumbatia kilimo cha kisasa na kutumia teknolojia pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo kujiajiri na kuanzisha biashara zao.
Lusaka amesema mabadiliko ya kilimo kutoka mfumo wa jadi kwenda kwenye kilimo cha kisasa yanaweza kuwapa vijana nafasi kubwa ya kushiriki katika uzalishaji, usindikaji, uuzaji na usafirishaji wa mazao, hivyo kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa ajira za kuajiriwa.
Viongozi hao wameeleza kuwa kuongezeka kwa ushiriki wa vijana katika kilimo kutasaidia kukabiliana na ukosefu wa ajira, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuimarisha uchumi wa taifa, huku teknolojia ikitarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kufanikisha mabadiliko hayo.
NA HARRISON KAZUNGU.